Maana Unayoipa Misamiati Ya Maisha Ndiyo Inayokupa Matokeo Unayoyapata.


Categories :

Mawasiliano binafsi au baina ya watu hujengwa na maneno ambayo yanaweza kuwa na maana tofauti. Maneno hayo huitwa misamiati. Misamiati hiyo inaweza ikawa na maana tofauti baina ya mtu na mtu. Watu wawili wanaweza wakatafsiri msamiati mmoja na wakatoka na maana mbili tofauti. Kwa sababu tafsiri za misamiati zinaamua vitendo anavyoweza kuchukua mtu, hii imekuwa sababu ya watu kuchukua vitendo tofauti na kupata matokeo tofauti pia.

Kuna misamiati ambayo umeipata tangu kuzaliwa kwako. Umeipa misamiati tafsiri kulingana na jamii ilivyokuwa inajitahidi kukutafsiria, ndiyo maana hata vitendo ambavyo umekuwa unavichukua vimeendana na vile jamii imekuwa ikivichukua. Kwa sababu ya kuchukua vitendo vinavyofanana, hujawa na maisha tofauti na jamii inayokuzunguka.

Maisha yako yatabadilika pale tu utakapoanza kutoa maana tofauti kwenye misamiati iliyopo kichwani mwako. Misamiati na maana ambazo zimetawala akili yako ndizo zinazoamua matokeo unayoyapata maishani mwako. Una misamiati gani na maana gani juu ya utajiri? Je una msamiati inawezekana akilini mwako, kama ndiyo ina maana gani? Nini maana ya afya kwako? Jifunze misamiati ifuatayo na jenga maana nzuri za misamiati hiyo ili uweze kubadili hatua unazochukua na kupata matokeo unayostahili.

MAFANIKIO: Huu ni msamiati unaoimbwa kila siku. Kila mtu atakwambia anatafuta mafanikio, mafanikio ni nini? Kila mtu amekuwa na maana tofauti ya mafanikio. Wengine wamefikiri mafanikio ni kuwa na fedha nyingi. Watu hawa wamewekeza nguvu kubwa kuhakikisha wanapata fedha, baada ya kupata fedha nyingi, wameendelea kuona kuna kitu bado wanapungukiwa. Sasa mafanikio ya kweli yana tafsiri gani? Kama ilivyo kwenye kifaa kinachotengenezwa kiwandani, mafanikio ya kifaa hicho itakuwa ni kuweza kufanya kazi iliyotegemewa ifanywe na kifaa hicho kwa ufanisi mkubwa na muda kamili; ndivyo ilivyo kwako, maana ya mafanikio kwako ni kutimiza kusudi uliloumbiwa. Kama bado hujaanza kuishi kusudi ujue bado hujaanza safari ya mafanikio.

UTAJIRI: Picha gani inakuja akilini mwako unapotaja au sikia neno utajiri. Kuna watu waliotafsiri utajiri kama kitu kibaya ambacho si kizuri kuwa nacho maishani. Wapo wanaoamini kuwa watu hawawezi kupata utajiri kwa njia halali, hivyo ni mpaka utumie njia za ushirikina au uwadhulumu watu wengine. Huwezi kupata utajiri kama msamiati huu una maana hasi kichwani mwako kwani utakuwa unaukimbia usikusogelee. Je unatafsiri utajiri kama kitu cha watu fulani, na wewe humo kwenye kundi hilo? Huwezi kuupata utajiri mpaka ubadili maana ya msamiati huu kichwani mwako. Utajiri ni  kitu kizuri kwani unaweza kutatua matatizo mengi yanayokusumbua na ya jamii pia. Utajiri ni haki ya kila mtu, na matajiri sio watu wabaya, bali tabia zao.

AFYA: Afya ni mtaji muhimu sana wa mafanikio ya maisha yako. Ili uweze kupata mafanikio makubwa unahitaji kuweka kazi kubwa na huwezi kuweka kazi kubwa kama afya yako si imara. Tofauti na afya ya mwili, kuna afya ya akili na roho pia. Nini maana ya msamiati afya kwako? Wapo wanaotafsiri afya kuwa ni kula chakula kingi au kuwa na kitambi . Afya ya mwili ni kuwa na mwili wenye kinga imara kuwezesha kustahimili magonjwa ambukizi, kula mlo kamili kwa viwango sahihi ambavyo havisababishi magonjwa yasiyo ya kuambukizwa. Pia inahusisha kufanya mazoezi na kupumzika kila siku.

HAIWEZEKANI: Je msamiati huu upo kichwani mwako. Huu ni miongoni mwa misamiati ambayo imetawala vichwa vya watu wengi. Umekuwa ukimaanisha kuwa jambo fulani haliwezi kufanyika au kutokea. Kuchukua hatua na kupata mafanikio kimekuwa ni kitu chenye maumivu na hivyo watu wengi hukwepa hilo kwa kusema haiwezekani. Ukisema haiwezekani inabaki haiwezekani kwani hakuna jitihada nyingine ambazo unaweza kuzichukua ili kuweza kupata matokeo. Unaweza kupata chochote unachokitaka duniani kama hakutakuwa msamiati HAIWEZEKANI akilini mwako.

WAJIBU: Huwezi kupata matokeo yoyote usipowajibika. Unahusika moja kwa moja kwenye matokeo ya maisha yako. Tafsiri gani unapata unapolitaja au sikia neno wajibu? Unawajibu wa kutengeneza mafanikio ya maisha yako. Hakuna mtu mwingine atakayewajibika na matokeo unayotarajia kuyapata. Chukua wajibu wa kujenga maisha yako kwa asilimia mia moja.

Ndugu! Hatua ya maisha uliyofikia imechangiwa sana na misamiati iliyojaa akilini mwako na tafsiri unazozitoa kwenye misamiati hiyo. Kama kuna maeneo ya maisha yako huridhiki na matokeo unayoyapata, basi anza kwanza kubadili misamiati na maana unayoipa misamiati hiyo. Anza kwa kufanyia kazi misamiati ya hapo juu kisha endelea kukagua mingine iliyopo akilini mwako.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *