Akili Yako Inahitaji Mazoezi Kama Misuli Yako Ili Ifanye Mambo Makubwa Zaidi


Categories :



Ili viungo na misuli yako iwe imara unahitaji kufanya mazoezi ya viungo. Mazoezi haya huhusisha kukimbia, kuruka, kunyanyua uzito nk. Wakati wa kufanya mazezi hayo mtu huhisi maumivu, kuashiria kuwa kitu unachokifanya ni nje ya mazoea ya mwili. Mazoezi hayo yakifanyika kwa uaminifu huwa na faida kubwa mwilini. Faida hizo ni pamoja na kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa, kupunguza msongo, na kuleta muonekano mzuri wa mwili. Faida nyingine ni mwili kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi.

Kama mwili unavyohitaji mazoezi ili kuwa imara na kufanya zaidi, ndivyo ilivyo kwa akili, ili uwezo wake ukue inahitaji mazoezi. Kumbuka mambo yote unayoyafanya huanza kama mawazo ambayo hutengenezwa akilini. Kumbe akili ni eneo muhimu sana la kuimarisha ili uweze kufikiri vema na kutenda kwa uaminifu.

Mazoea ya akili si ya kunyanyua uzito au kukimbia bali ni ya kuifanya akili yako ifikiri zaidi ya ulivyozoea. Unapoipa akili yako mazoezi unaifanya itengeneze mtandao mpya wa kuchakata taarifa. Kadri akili yako inavyofanya mazoezi ndivyo inavyoimarika na kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha mawazo bora na kutatua changamoto hata kubwa. Zifutazo ni njia ambazo unazoweza kutumia kufanyisha mazoezi akili yako huku ukipata faida kubwa katika maisha yako;

Muda maalumu wa kufikiri. Ili uweze kufanya mazoezi ya misuli na viungo unahitaji muda maalumu wa kufanya mazoezi. Mara nyingi watu hufanya mazoezi asubuhi au jioni. Ili uweze kufanya mazoezi ya kufikiri na kulipa zoezi hilo uzito

Toka nje ya mazoea. Mtu anapojifunza kuendesha baiskeli au gari huishirikisha akili yake sana. Kila wakati atafikiri ni kitu gani sahihi anapaswa kukifanya. Katika hatua hii huwa hapendi hata kuongeleshwa kwani anajua anayemuongelesha anatoa umakini wake. Lakini akishazoea, hafikiri tena kwa kina wala kuweka umakini kama mwanzo. Hivyo ndivyo inavyotokea pale unapofanya vitu kimazoea. Huwezi kufanyisha mazoezi akili yako kwa kufanya vitu kimazoea. Hata kama unafanya kitu kile kile, fikiri ni kwa namna gani leo unaweza ukakifanya kwa ubora kuliko jana.

Weka malengo makubwa. Unapokuwa na malengo makubwa utahitaji kufikiri zaidi ili uweze kufanikiwa kuyatekeleza. Malengo makubwa yatakulazimisha ufikiri nje ya kisanduku na ndipo unapoiumiza akili yako kutanuka na kuwa imara zaidi. Baada ya kukamilisha lengo la kwanza, panga kubwa zaidi ya lile.

Usizikimbie changamoto badala yake zikabili. Changamoto za maisha zipo kila siku, je unazikimbia au unazikabili. Ukiikabili changamoto unaipa akili yako kufikiri zaidi ya pale ilipokuwa na hivyo kuijengea uwezo wa kwenda mbali zaidi. Kwa sababu thamani hupatikana kwa kutatua changamoto, kadri unavyoizowesha akili yako kutatua changamoto kubwa ndivyo unatengeneza thamani kubwa kwa watu wengine na hivyo kutengeneza utajiri wako.

Fanya mambo ya kukufikirisha. Ipe akili yako mazoezi kwa kufanya vitu ambavyo vitakufanya ufikiri. Kusoma kitabu kunafanya akili yako ifikiri kuliko kuangalia runinga. Hakikisha una utaratibu wa kusoma angalau kurasa kumi za kitabu kila siku.

Akili yako inahitaji mazoezi ili iweze kuimarika na kufanya mazoezi. Fanyisha akili yako mazoezi hayo hapo juu mara kwa mara ili uzidi kuimarika na kufanya mambo makubwa zaidi.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *