Unachokifanya Sasa Ndicho Kinachoamua Mafanikio Ya Maisha Yako.


Categories :


Ukiwa katikati ya jangwa, ukiangalia nyuma hutaona mwanzo wake, ukiangalia mbele hutaona mwisho wake. Sehemu pekee unayoweza kuiona ni pale utakapokuwepo. Maamuzi yako ya kitu gani ukifanye yatategemea vile unavyoviona kwa muda ule.

Maisha yako yamegawanyika sehemu tatu; yaliyopita, yaliyopo na yajayo. Mambo uliyoyafanya wakati uliopita ndiyo yaliyokupa maisha ya sasa. Mambo unayoyafanya sasa ndiyo yatakayoamua maisha yako yajayo.

Huna uthibiti wowote kwenye maisha yako yaliyopita. Kama kuna makosa uliyoyafanya, huwezi kubadili chochote zaidi ya kujifunza kutokana na maisha hayo. Maisha yako yajayo, hata ya kesho huna uthibiti kwa sababu bado hujayagusa. Licha ya kuwa na mipango mingi mkononi mwako lakini huna uhakika wa asilimia mia moja kuwa itakuwa kama ulivyopanga.

Wakati uliopo yaani leo ndiyo ambao upo mikononi mwako. Leo ndiyo unaweza kuipangilia vizuri na kufanya mambo ambayo yataleta matokeo ya maisha unayotarajia. Si jana wala kesho bali leo. Hivi ndivyo unavyoweza kuiishi leo kwa faida;

Usijinyong’onyeshe na yaliyopita. Jambo lililokwisha huna uthibiti nalo. Hakuna unachoweza kubadili kwenye jambo ambalo limekwisha tokea. Faida pekee unayoweza kuipata kutokana na mambo ambayo yamekwishatokea ni kujifunza pekee. Usiruhusu mambo yaliyopita yaathiri utendaji wako wa sasa. Usinung’unike, wala kulalamika kwa ajili ya mambo ambayo yamekwisha tukio. Jikite leo kuhakikisha unaitumia vizuri siku ya leo kujenga kesho yako badala ya kuangalia mambo yaliyopita ambayo hayana umuhimu wowote.

Iishi leo kikamilifu. Leo ndiyo muda pekee amabo una uhakika nao wa kufanya unachokitaka. Huu ni muda unaoweza kupanga na kufanya kwa ajili ya muda ujao. Nini unataka kitokee maishani mwako? Leo ndiyo siku pekee ya kukifanya hicho. Kabla hujaanza siku yako, hakikisha unaipangilia vizuri, kujua nini utakifanya na weka nidhamu kuhakikisha unakifanya. Mwisho wa siku fanya tathmini kuona ni kwa kiasi gani umetekeleza yale uliyopanga kufanya siku hiyo. Ili kukua na kufikia mafanikio makubwa hakikisha angalau unatekeleza 80% ya yale uliyoyapanga.

Weka mipango ya muda ujao lakini anza kuiishi leo. Malengo ya muda ujao ndiyo yanayobeba mwelekeo wa maisha yako. Haya huwa ni malengo makubwa yanayohitaji muda mwingi. Lakini ili malengo haya yatimie huna budi kuyagawa malengo yako makubwa mpaka kwenye mipango unayoweza kutekeleza kwenye siku. Gawa malengo yako mkubwa kwenye vipande na yatekeleze kikamilifu, ndipo unapoweza kufikia mafanikio makubwa unayotarajia.

Furahi kila leo. Imekuwa kasumba ya watu wengi kusubiri matokeo fulani ndipo afurahi. Matokeo huchukua muda mrefu kutimia na kisha kudumu kwa muda mfupi. Njia ya uhakika ya kuwa na furaha maishani mwako wakati ukisaka mafanikio ni kufurahia mchakato. Furahia chochote unachokifanya ambacho kitapelekea matokeo unayoyataka. Ishi mchakato kila siku, furahi kila siku. Hii ndiyo itakuwa hamasa kwako kupiga hatua.

Usiihofie kesho. Hofu ya kutopata matokeo yanayotarajiwa imekuwa kikwazo cha watu kutochukua hatua. Itakuwaje kama nitashindwa? Watu watanionaje? Je watu hawatafikiri sina uwezo? Haya yamekuwa ni mawazo ambayo yamekufanya usichukue hatua leo kwa sababu ya kuhofia kesho. Waliofanikiwa waliishinda hofu hii kwa kutoogopa kushindwa. Walijiua ni afadhari ukafanya ukashindwa kuliko kutokufanya. Usiache kuchukua hatua leo kwa hofu ya kushindwa. Fanya kwa viwango vya juu kisha acha asili iamue. Mara nyingi itakuwa upande wako.

Mafanikio unayoyataka maishani mwako yanaamuliwa na unachofanya leo, tena sasa. Baada ya kujua nini unakitaka maishani mwako, gawa malengo yako na kuhakikisha kila siku una kitu cha kufanya juu ya malengo yako.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *