Makosa Matano (5) Uliyoyafanya Kwa Kufikiri Dunia Ina Uhaba


Categories :

Ukichoma msitu na kuteketeza chochote kilichopo, baada ya muda majani na miti itaota tena na kutengeneza msitu mwingine. Binadamu wamekuwa wakivua na kula samaki baharini kwa miaka mingi, lakini bahari haijawahi kuishiwa samaki. Binadamu wamekuwa wakivuta hewa kwa miaka mingi na idadi yao imekuwa ikiongezeka lakini hakuna hata siku moja tumeshuhudia dunia ikiishiwa hewa. Hii ni mifano michache tu kati ya mingi ambayo inadhihirisha kuwa dunia ina utele wa vitu.

Watu wengi kwa sababu ya historia na makuzi mbalimbali wamekuwa wakifikiri kuwa dunia ina uhaba. Kwa kufikiri hivyo wameamini vitu fulani vimeshashikiliwa na watu wengine na wao hawawezi kuvipata tena. Imekuwa rahisi kuamini kuwa kwa sababu watu fulani ni matajiri, ni vigumu na wewe kuwa tajiri. Au kwa sababu mtu fulani ana mali nyingi ni vigumu na wewe kuwa na mali nyingi. Hizi ni fikra za kuamini watu fulani wamechukua vingi na kwa sababu dunia ina uhaba, wewe utapata kidogo au hutapata kabisa.

Mawazo ya uhaba ndiyo yaliyokufikisha kwenye hali ya maisha uliyonayo sasa. Mawazo hayo yanaathiri sana hatua unazochukua kila siku. Hatua unazochukua tangu kujipangia kiasi cha mafanikio unayoyataka kuyapata yanategemea sana unaionaje dunia, ina utele au uhaba? Kwa kufikiri na kuamini dunia ina uhaba, umefanya makosa yafuatayo ambayo yamepelekea matokeo ya maisha uliyonayo leo;

Umeamua kuishi ndoto ndogo. Huwezi kufikiri kupata makubwa kama unaamini dunia ina uhaba. Kwa kufikiri dunia ina uhaba hujaamini kama unaweza kupata vitu vikubwa maishani mwako. Ndoto ndogo uliyonayo imetokana na jinsi ulivyoikadiria kiasi ambacho dunia inacho kwenye kile unachokitaka. Umejiwekea ndoto ya kuwa na fedha kidogo baada ya kuamini kuwa wewe umechelewa na fedha nyingi zilishachukuliwa na waliowahi. Dunia ina kiasi kikubwa cha kile unachotaka. Fikiri upya sasa, dunia ina utele, unaweza kupata chochote unachokitaka.

Uvivu. Baada ya kuamini kuwa dunia ina uhaba, ukabweteka na kuona huna kitu kikubwa cha kufanya. Kufikiri dunia ina uhaba kumekupunguzia hamasa ya kuweka kazi kubwa ili kupata matokeo makubwa. Umeamini kuwa hata ukifanya kazi kwa bidii hutapata vingi kwa sababu vingi vimeshachukuliwa. Amua leo nini unataka, weka kazi kubwa dunia ina utele na nguvu zako hazitaenda bure.

Umeishi kwa kuiga watu wengine. Ulipofikiri dunia ina uhaba, ukapoteza ubunifu wako baada ya kuona hakuna wazo jipya unaloweza kulibuni. Umeamini kuwa mawazo yote mazuri ya biashara yalishabuniwa na watu wengine. Umesahau kuwa wewe ni mtu wa pekee na una upekee ndani yako wa kubuni kitu cha kipekee. Dunia ina utele wa mawazo na mengine yapo ndani yako, huna haja ya kuiga maisha ya mtu mwingine bali ishi upekee wako.

Umeshindwa kuuamsha uwezo wako. Ndani yako kila mtu ikiwa ni pamoja  na wewe kuna nguvu kubwa ambayo bado haijatumika. Nguvu hii ikiamshwa inaweza kufanya mambo makubwa na kupata matokeo makubwa. Kwa kufikiri dunia ina uhaba, ni sawa na kuubembeleza uwezo huo kuendelea kulala. Fikiri kinyume chake leo, una utele wa uwezo ndani yako upangie malengo makubwa nao utakuwa tayari kukutimizia.

Umetengeneza chuki. Sababu mojawapo ya masikini kuona matajiri ni watu wabaya ni kwa sababu ya kufikiri dunia ina uhaba. Masikini anayefikiri dunia ina uhaba ataamini kuwa  yeye hana fedha au mali kwa sababu tajiri amechukua vyote. Hii imewafanya masikini wawachukie matajiri. Matajiri ni watu wazuri, wafurahie na kuwapenda kwani ukikaa nao karibu watakubadilisha mtazamo na utaona dunia bado ina utajiri mwingi ambao na wewe unaweza kuuchota.

Ndugu! Kuna mabadiliko makubwa yatatokea kwenye maisha yako pale utakapoanza kuamini kuwa dunia ina utele. Dunia haina uhaba, tumia utele wa uwezo mkubwa ulio ndani yako kupata chochote kwa kiasi chochote ambacho dunia tayari inacho. Tengeneza ndoto kubwa kisha weka mipango ya kuiishi ndoto hiyo mpaka itimie. Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI kimeeleza kiundani ni kwa namna gani unaweza kupata chochote kwenye dunia yenye utele kwa kuamsha uwezo wako ambao tayari upo ndani yako. Jipatie nakala yako leo kwa kupiga simu namba 0752 206 899 ili uanze kuufaidi utele wa dunia hii.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *