Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuendesha Maisha Yako Hata Kwenye Wingu Zito.


Categories :



Rubani huweza kuiongoza ndege hata kwenye wingu zito, si kwa sababu ana uwezo wa kuona mbele, bali kwa sababu ana dira inayomuongoza wapi aielekeze ndege hiyo. Licha ya mawimbi mazito na giza kubwa ambalo linaweza kutanda asione mbele lakini huenda kwenye uelekeo sahihi kwa sababu ya dira inayomuongoza.

Mtu ambaye ni mwenyeji  anayetembea usiku kwenye giza nene yupo kwenye nafasi ya kufika nyumbani salama, si kwa sababu macho yake yanaiona njia, bali kwa sababu akili yake inaifahamu njia. Hata kama macho yake hayaioni njia, akili yake inaweza kukadiria kuwa inakaribia kufika nyumbani na kukumbuka kuwa sehemu fulani kuna shimo analotakiwa kuliruka au kulikwepa.

Maisha ya mafanikio makubwa ni sawa na kuendesha ndege angani ambapo kama rubani anavyokutana na machafuko ya anga, ndivyo na msaka mafanikio anavyoweza kukutana na changamoto ambazo kwa mtazamo wa kawaida hutaweza kuona njia ya kupiga hatua. Ndiyo maana umeshawahi kuwasikia watu wakisema sioni cha kufanya, naona nimefika mwisho. Mwisho wa watu hawa huwa ni kukata tamaa na kurudi nyuma.

Kama rubani anavyoweza kuendelea kuendesha ndege hata kwenye wingu nene, au mwenyeji kurudi nyumbani hata wakati wa giza nene, ndivyo hata msaka mafanikio unavyotakiwa kuendelea kupiga hatua hata pale unapokuwa umegubikwa na wingu zito la changamoto. Kuna dira na ramani unazopaswa kuwa nazo ndani yako ili uweze kusonga mbele na kufikia mafanikio pale unapokutana na changamoto mbalimbali. Dira na ramani hizo unaweza kuzijenga kama ifuatavyo;

 
Kusudi. Kinachoifanya ndege iweze kutembea hata kwenye wingi zito ni kusudi lake. Aliyeitengeneza alitambua wazi kuwa anga litachafuka na hivyo kuipa uwezo ndege hiyo wa kutembea hata kwenye wingu zito ili kutimiza kusudi lake la kusafiri angani. Pale unapofanikiwa kuishi kusudi lako ndipo unapokuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto zozote zile utakazokutana nazo ili uweze kutimiza kusudi hilo. Uliletwa duniani kukamilisha kusudi fulani na huku ukiwa na uwezo mahususi wa kuzikabili changamoto zozote zile ili kulikamilisha kusudi hilo. Tafuta mafanikio kwa kutimiza kusudi lako ndipo utakapofanikiwa kuendesha maisha yako hata kwenye wingu zito.

Ndoto. Mtu huweza kuona picha na mwendo wa vitu wakati wa usiku akiwa amelala. Huziona picha si kwa macho bali kwa akili yake. Kuna ndoto ambayo msaka mafanikio unatakiwa uitengeneze, hii ni ndoto unayoweza kuiota hata mchana ukiwa macho. Ndoto hii ni jambo kubwa ambalo unatamani kulikamilisha na kuacha alama kabla hujaiacha dunia. Ndoto hii hutawala akili yako usiku na mchana. Ukiitengeneza ndoto hii utaweza kuona njia hata mbele ya wingu zito.

Hamasa ya kudumu. Unapokutana na changamoto ni rahisi sana kukata tamaa. Mafanikio makubwa hukutana na changamoto nyingi tena kubwa. Katika mazingira haya unahitaji hamasa ya kudumu ya kukuwezesha kusonga mbele hata kama kwenye wingu zito. Kutambua kusudi lako, kuwa na ndoto kubwa, kuwa na kwa nini kubwa ya kufanya jambo fulani huweza kukupa hamasa kubwa ya kuendelea kuchukua hatua  hata pale unapokuwa kwenye wingu zito la changamoto.

Hakuna mafanikio makubwa yasiyo na changamoto kubwa. Unahitaji kujiandaa kuendelea kupiga hatua hata pale unapokutana na changamoto. Anza kujenga dira hizo tatu zitakazokusaidia kukabiliana na changamoto kubwa na kufikia mafanikio makubwa.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *