Tengeneza Tabia Hizi Tano(5) Ili Kuanza Kutengeneza Mafanikio Yako
Hakuna kitu chochote kinachoweza kutokea bila kuweka kazi. Unafanya kazi kwa kupanda gari la tabia. Kuna watu wamepanda gari hili na kufikia mafanikio makubwa. Lakini wapo waliopanda gari hili na kuishia njiani. Wapo waliopanda hili hawajaianza safari mpaka sasa.
Kuishi maisha yako kwa mafanikio kunategemea tabia ulizozitengeneza na kuziishi. Je umepanda gari gani? Gari ulilolipanda limeanza safari? Kama limeanza safari limefika wapi? Kasi ya mafanikio yako inategemea kasi ya gari la mafanikio ulilolipanda. Kufika safari au kutofika kutategemea gari ulilolipanda pia. Bahati mbaya au nzuri ni kuwa kila mtu yupo kwenye gari la tabia, hakuna mtu anayeweza kuishi bila tabia. Hivo hivyo hakuna mtu anayeweza kufanikiwa au kushindwa bila kuwa na tabia.
Tofauti ya aliyefanikiwa na aliyeshindwa ipo kwenye tabia alizozitengeneza. Jambo la kwanza ambalo unapaswa kulitazama baada ya kukosa mafanikio kwa muda mrefu ni tabia. Je unaishi tabia za mafanikio au hapana. Uzuri ni kwamba tabia za mafanikio zinafahamika na unaweza kuziishi na kuyapata mafanikio kama watu wengine. Waliofanikiwa walizitambua tabia ambazo walipaswa wazijenge, wakazijenga na kisha kuziishi. Naenda kukushirikisha tabia tano ambazo unaweza kuanza kuzijenga sasa ili kufikia mafanikio yako.
1. Kuwa na malengo unayofanyia kazi. Melengo ni dira ya nini unafanya maishani mwako. Bila kuwa na malengo huwezi kujua wapi unaelekea. Kama hujui unakoelekea huwezi kufahamu kama unapotea. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa lazima ujenge tabia ya kuweka malengo na kuyatimiza.
2. Ipangilie siku yako. Malengo ya mtu hutimizwa kwa hatua anazozichukua kila siku. Utafanikiwa kuiishi siku yako vizuri kisha kufikia mafanikio kwa kujenga tabia ya kuipangilia siku yako. Unapoimaliza leo au kabla hujaianza kesho panga na tambua kwa hakika ni kitu gani unaenda kukifanya.
3. Kuweka akiba. Ni ndoto ya watu wengi kuwa huru kifedha. Hii ni hatua ambayo fedha inakuwa sio sababu ya kutofanya kitu fulani unachokipenda. Hatua hii utaweza kuifikia kwa kujijengea tabia ya kuweka akiba kwenye kila kipato unachokipata na kuiwekeza akiba hiyo. Anza kutenga angalau asilimia kumi ya kila kipato unachokipata.
4. Kuamka mapema. Kuiishi kikamilifu ni pamoja na kuianza siku vizuri. Unaweza kuianza siku vizuri kwa kuwahi kuamka. Unapowahi kuamka unapata muda tulivu wa kufanya mambo muhimu kabla ya kuwa na usumbufu mwingi. Unapowahi kuamka unakuwa muda maalumu kwako. Kwenye muda huu maalumu unaweza kuipangilia siku yako, kuandika malengo yako, kusoma, kusali, kutahajudi na kuandika. Tengeneza tabia hii ya kuamka mapema kabla ya watu wengine ili uweze kupiga hatua.
5. Ustahimilivu. Safari ya mafanikio haijawahi kuwa rahisi. Ina milima na mabonde ya changamoto nyingi kabla ya kufika kilele. Safari ya mafanikio huanza na watu wengi, lakini wanaofika mwisho ni wachache kwa sababu ya changamoto zenye maumivu zinazotokea njiani. Safari ya mafanikio inakuhitaji ujenge tabia ya ustahimilivu ili uweze kusimama pale unapoanguka, uweze kuvumilia unapokutana na maumivu na kuweza kusubiria matokeo pale yanapochelewa.
Ndugu! Mafanikio ni tabia, pale unapofanikiwa kutengeneza tabia nzuri za mafanikio zinakuwa kama gari linaloweza kukuanzishia na kikufikisha kwenye safari yako ya mafanikio. Anza kutengeneza tabia hizi na kuziishi ili uweze kufikia mafanikio unayoyatarajia.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz