Geuza Sarafu Yako Kuuona Upande Mwingine Wa Maisha Yako.
Sarafu ina pande mbili, upande wa kichwa na upande wa mkia. Lakini mara nyingi huwa tunaweza kuuona upande mmoja tu kwa wakati. Ukiona unauona upande mmoja ujue upande mwingine umejificha. Kama upande unaoonekana kwa muda huo sio ule unaoutaka unaweza ukaigeuza sarafu yako kupata upande ule unaoutaka.
Matokeo ya maisha yako yana pande mbili. Kwenye matokeo unayoyaona sasa kuna upande mwingine. Kwa hiyo kama una matokeo unayapata sasa, tambua kuwa kuna matokeo kinyume na hayo unayoweza kuyapata. Kwa sababu matokeo yanatokea kwa kufanya kitu, kumbe ili uweze kupata matokeo tofauti inakupasa kufanya kwa utofauti pia.
Kuna matokeo gani unayapata sasa lakini hayakupendezi? Kuna tabia gani unaifanya sasa lakini inakuudhi? Kuna kiasi gani unakipata sasa lakini huridhiki nacho? Je una watu wa karibu lakini unaona hawakusaidii kufika safari yako? Kumbuka majibu ya maswali haya unayojiuliza ni matokeo ya vile unavyofanya sasa. Kama ni matokeo ambayo hupendezwi nayo, unaweza kubadili vitendo vyake na kupata yale yanayokuridhisha na yatakayokupeleka kwenye mafanikio makubwa. Yafuatayo ni mambo unayoyafanya sasa na yaliyokupa matokeo ya sasa na upande mwingine ambao unaweza kufanya kupata matokeo yatakayokufikisha unakotaka kufika;
Uvivu na Bidii. Hizi ni pande mbili ambazo zinakupa matokeo tofauti. Kama hupatia matokeo madogo inawezekana huweki kazi kubwa kwenye mambo unayoyafanya. Mafanikio makubwa yanahitaji kufanya kazi kwa bidii. Wale wanaoweka kazi kubwa mahali sahihi wanapata matokeo makubwa. Kinyume cha uvivu ni bidii. Weka bidii kwa kuweka kazi kubwa kwenye mipango yako mizuri ili uanze kupata matokeo mazuri.
Kuahirisha vs kufanya. Mipango siyo matumizi. Hii ni kauli ambayo hudhihirika pale muda wa utekelezaji unapofika. Watu wengi ni wazuri kwenye kuweka malengo lakini sio kwenye utekelezaji. Kila mtu anaweza kupanga afanye nini, lakini wengi wamekuwa na tabia ya kuahirisha mambo waliyoyapanga. Kama umekuwa hupati matokeo unayoyataka, jiulize kama umefanya vitu kama ulivyopanga? Je husemi utafanya kesho vile unavyotakiwa uvifanye leo? Una nafasi ya kuangalia upande mwingine wa shilingi. Acha kuahirisha mambo na anza kujisukuma kufanya vitu kama unavyopanga.
Kuhuzunika na kufurahi. Kuna mambo yanatokea katika maisha ya wanadamu, kuhuzunisha au kufurahisha vinategemea na tafsiri ya mtu. Kwenye kila jambo ambalo unafikiri linahuzunisha, kuna upande mwingine wa shilingi ambao unafurahisha. Kama upo kwenye huzuni jaribu kugeuza upande mwingine wa shilingi utaona kitu kinachofurahisha.
Utajiri na Umasikini. Utajiri na umasikini ndiyo imekuwa agenda kuu ya watu hapa duniani. Utajiri umekuwa tamanio la watu wengi hapa duniani. Lakini uhalisia ni kwamba kuna idadi ndogo tu ya watu waliofanikiwa kufikia utajiri. Kama upo upande wa umasikini, unaweza kugeuza upande mwingine wa shilingi na kuuona utajiri. Kugeuza shilingi na kuuona utajiri unakuhitaji kubadili yale unayoyafanya sasa ambayo yamekupa umasikini. Unaweza kuigeuza shilingi na kuuona utajiri kwa kuongeza thamani zaidi kwenye vile unavyofanya, kuanza kuweka akiba kwenye kila kipato na kukiwekeza zaidi na kutumia chini ya kipato chako.
Kulalamika na Kuwajibika. Kuna hali ngumu za maisha huwa zinakutokea na kukushwishi kuwa kuna mtu anayesababisha. Ni rahisi sana katika hali kama hiyo kuona kuna watu waliohusika kutengeneza hali hiyo isiyokuridhisha. Kwa mfano mtu anapokuwa masikini au kuwa na kipato kidogo, au changamoto kwenye biashara ni rahisi sana kuilaumu serikali. Mafanikio ya maisha yako ni wajibu wako. Huwezi kupata mafanikio kwa kulalamika. Anza kuwajibika kwa kila hatua ya maisha yako huku ukiacha kulalamika.
Ndugu! Upo kwenye hali gani sasa? Hali hiyo unaweza kuibadili kwa kugeuza shilingi upande mwingine huku ukibadili vile unavyofanya. Anza kugeuza shilingi leo kwa kuacha unayoyafanya sasa kufanya mambo hayo matano ya upande mwingine wa shilingi yaliyoorodheshwa hapo juu.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz