Usibaki Unasubiri! Nenda Kalipie, Huduma Ya Mafanikio Yako Ni Ya “Lipa Kwanza”


Categories :



Huwezi kwenda benki na kupanga foleni ya kwenda kutoa fedha kwenye mashine huku ukijua huna fedha yoyote kwenye akaunti yako. Pia huwezi ukatunga namba zozote zile kisha kuingiza kwenye mita ya umeme huku ukitambua kwamba ilikupasa ulipie fedha kisha upate namba za luku kwenye mita yako ili upate umeme. Kadhalika muda wa mavuno ukifika huwezi kwenda kwenye shamba ambalo hukupanda chochote kwa lengo la kuvuna mazao.

Nakupongeza sana kwa kuwa mwerevu na kutambua kuwa huwezi kupata huduma hizo bila kulipia kwanza pia kuvuna shamba bila kupanda chochote. Lakini nina swali kwako kuhusu mavuno ya mafanikio yako yaani yale uliyotamani. Mbona unataka kupata mafanikio hayo bila ya kulipia kwanza? Mbona unataka kuvuna mafanikio hayo bila ya kupanda kwanza?

Mafanikio yako yanafuata sheria ya asili kuwa kwenye kila matokeo unayoyaona kuna kisababishi cha matokeo hayo. Kisababishi kinatokea kabla ya matokeo. Hivyo kutaka matokeo kwanza kabla ya kuweka kisababishi ni kwenda kinyume na sheria ya asili.

Mwaka huu ulipokuwa unaanza, watu wengi, inawezekana na wewe waliweka malengo ya nini wanataka wakipate mwaka huu. Hamasa ilikuwa juu sana, lakini jiulize mwenyewe ni kwa kiasi gani umeshaanza kutekeleza malengo yako ikiwa ni zaidi mwezi mmoja sasa tangu uyaweke? Kuna uwezekano mkubwa kuwa mpaka kufikia mwezi Juni, watu wengi watakuwa hawajui nini walikipanga. Matokeo unayotarajia kuyapata mwaka huu kupitia malengo yako ni huduma ya lipa kwanza. Utakapoweka kazi, nidhamu na ustahimilivu ndipo utakapoyapata matokeo hayo na si vinginevyo.

Mtu pekee wa kulipa kwanza gharama kwa ajili ya mafanikio yako ni wewe mwenyewe. Kwa nini unafikiri serikali au wazazi ndiyo wa kukupatia kile unachokitaka? Mara nyingine umeingia kwenye mtego kwa kufikiri kuwa utakipata unachokitaka kwa bahati, yaani utalala masikini na kuamka tajiri. Nakukumbusha huduma hii ya mafanikio yako kama vile utajiri, afya njema nk vinapatikana kwa kulipia kwanza, kupitia kazi na ustahimilivu.

Inawezekana kuna vitu tayari unavifanya kwa muda mrefu sasa lakini umekuwa ukipata matokeo yaleyale, unaendelea kujifariji kuwa kuna siku mambo yatakuwa mazuri. Ndugu! Albert Einstein alisema “Insanity is doing the same thing over and over and expecting different results.” akimaanisha kuwa wazimu ni kuendelea kufanya kitu kile kile kwa namna ileile huku ukitarajia kupata matokeo tofauti. Ili uweze kupata matokeo bora zaidi lazima ufanye bora zaidi. Ili uweze kupata faida kubwa zaidi ya unayopata sasa kwenye biashara lazima uongeze mauzo zaidi hakuna njia ya mkato.

Asili ipo kukusaidia kwenye kile unachofanya. Mvua peke yake haiwezi kukupa mavuno kama hujapanda chochote shambani. Weka kazi kwanza kabla hujataka matokeo. Utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kukutana na bahati kama kutakuwa na maandalizi unayoyafanya.

Unataka nini kwenye maisha yako? Dunia ina kila kitu unachokitaka maishani mwako na inaweza kukupa chochote kwa kiasi chochote. Kwa nini hujapata mpaka sasa, ni kwa sababu bado hujalipia. Umetaka upate huduma hiyo ndipo ulipie ambapo si sahihi. Ainisha leo kitu kimoja kwenye kila eneo muhimu la maisha yako (Afya, binafsi fedha, kazi, mahusiano) kisha ainisha gharama unazotakiwa kulipa kwanza ili kupata matokeo hayo. Baada ya kuainisha gharama hizo, chukua jukumu mwenyewe la kuzilipa ndipo utapata chochote unachotaka.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *