Hii Ni Siri Ya Kupata Chochote Unachotaka Unayoweza Kujifunza Kwa Mtu Aliyekuwa Anakaribia Kufa Maji.
Kuna mtu mmoja alienda kuogelea ufukweni kama watu wengi wanavyoweza kwenda na kufanya hivyo. Alianza kwa kuogelea kwenye kina kifupi lakini kadri utamu wa maji ulivyozidi kuongezeka ndivyo alivyozidi kusogea kwenye kina kirefu bila kujua. Akiwa kwenye kina kirefu hali ya bahari ikachafuka na kuanza kukosa uwezo wa kuogelea vyema. Hali ilivyozidi kuwa mbaya, ikabidi aanze kupiga kelele kuomba msaada. Lakini mpaka watu wa kumuokoa walipofika, alikuwa ameshazama mara kadhaa na kukosa hewa na kunywa maji. Waokoaji walifanikiwa kumtoa nje ya maji na kumpa huduma ya kwanza akiwa hoi na kupumua kwa shida sana.
Baada ya kumsaidia na kisha kupata fahamu, mhanga huyo aliwaeleza nini kilitokea kwenye ajali aliyoipata. Lakini kuna jambo moja ambalo alilisema ambalo alijifunza, ni muhimu sana katika maisha yako ili kuweza kufikia mafanikio makubwa kwa kupata chochote unachokitaka. Na wewe unaweza kujifunza hicho na kikakusaidia maishani mwako. Alisema hivi; wakati anazama majini na kuibuka muda huo alikuwa hakumbuki chakula kizuri alichoacha kinapikwa nyumbani, alikuwa hafikirii atawapataje marafiki zake ili waende kula starehe, hakukumbuka siku hiyo kama klabu ya mpira anayoishabikia kama ilikuwa inacheza, wala hakuona zile fedha zilizokuwa benki zilikuwa na thamani kwake…..
Alisema kuna kitu kimoja tu ambacho kilikuwa na thamani kubwa kwake na jitihada zote zilikuwa kukipata hicho. Yaani akili, mwili, umakini nk vilikuwa vikihangaika kupata hicho tu. Kitu hicho ni hewa. Kila jitihada iliyofanywa ilikuwa ni ya kupata hewa tu. Hakuna kitu kingine kilichokuwa na thamani kama hewa kwa muda huo. Alipokuwa anazama kichwa alifanya kila kinachowezekana kuibua kichwa chake juu ya maji ili apate hewa. Bila hewa aliona kifo kikiwa machoni pake.
Ndugu! Kuna somo kubwa sana hapa ambalo unaweza kujifunza na kulitumia kupata mafanikio makubwa. Unaweza kupata chochote hapa duniani kama utafikia hali ambayo mhanga huyu aliyekuwa anataka kufa maji aliyoifikia. Utakipata chochote kama utafanikiwa kutengeneza kiu kubwa sana ya kukipata kitu hicho. Hii ni sababu mojawapo ambayo watu wameshindwa kuvipata vitu wanavyovitaka. Wanazama kwenye maji lakini bado wanafikiri chakula kizuri nyumbani, bado wanawaza fedha zilizopo benki, wanawaza ushabiki walionao, bado wanawalalamikia watu waliowakosea nk. Katika hali hii huwezi kuwekeza kila kitu kupa hewa.
Utafikia hali hiyo hapo juu kwa kuwa na KWA NINI kubwa inayoshinda vishawishi na changamoto zote. Ukifanikiwa kujenga kwa nini kubwa ya kupata kitu fulani upo kwenye nafasi kubwa ya kukipata. Kuna watu walioanza kujenga na kumaliza nyumba za kuishi hata kama walikuwa na kipato kidogo, baada ya kunyanyaswa sana na wenye nyumba. Walifika hatua na kujiuliza kwa nini naendelea kunyanyasika kiasi hiki? Kwa nini nisijenge nyumba yangu? Wapo wanafunzi walioweka jitihada kubwa za kusoma shule kwa bidii na kupata ufaulu mkubwa baada ya kuona namna wazazi au walezi walivyokuwa wanapata shida kulipa gharama kwa kuwa na kipato kidogo.
Hujaziona kwa nini kubwa kwako kwa sababu ya kujifariji na kuuficha ukweli wa maisha yako. Au kwa sababu umekwepa kuchukua jukumu la maisha yako kwa kuona kuna mtu mwingine anayeweza kuyaishi maisha yako kwa niaba. Wazazi na walezi wengi wamehangaika sana kupata fedha za kulipa ada za shule mwezi Januari zilipokuwa zinafungua shule kwa sababu ya kuwa na kipato kidogo. Wengine wamelazimika kukopa mikopo yenye riba kubwa ili waweze kuzikabili gharama hizo. Kuna wengine wameishi maisha magumu sana, wanasema maisha ya kuunga unga ili kukusanya fedha na kulipa ada. Kaa chini na tafakari vizuri, hii inaweza kuwa kwa nini ya kutosha ya kuanza kuongeza kipato.
Eneo gani la maisha linakukosesha raha ya maisha? Je ni kipato kidogo? Lifanye jambo hilo kuwa hewa unayoitafuta ukiwa unazama majini. Wekeza nguvu zako zote, akili yako yote, muda wako wote wa mwaka huu. Kama mtu alikuwa anazama kutoona haja ya chakula kwa muda huo, starehe, au fedha ndivyo na wewe unavyotakiwa kuona kuwa mwaka huu unahitaji hicho tu, acha kuhangaika na fursa nyingine zama kwenye jambo hilo, muda utafika na utalipata tu.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz