Hivi Ndivyo Unavyoweza Kupiga Hatua Kubwa Kwa Kuweka Tu Tarehe Ya Mwisho; “Deadline”.
Wanamichezo wameshuhudiwa wakiwa na hamasa kubwa na kujiandaa kwa nguvu na umakini mkubwa zaidi siku chache kabla ya mashindano kuliko mwanzo hata kama walikuwa wanafahamu ratiba hiyo kwa muda mrefu. Wanafunzi wameshuhudiwa wakiwa na umakini zaidi, kutumia muda mwingi zaidi wa kujiandaa siku chache kabla ya mtihani hata kama ratiba hiyo ilitoka muda mrefu. Inasemekana pia hata uelewa wao huwa mkubwa pale mtihani unapokaribia. Hata kwenye makampuni inaonyesha kuwa utendaji wa wanafanyakazi huwa vizuri zaidi mwishoni mwa robo ya msimu ikiwa ndiyo muda wa kufanya tathmini.
Kuna mifano mingi ambayo ningeweza kuendelea kuitoa hapo juu. Lakini mifano yote hiyo inaonyesha ni kwa namna gani utendaji wa binadamu unakuwa mkubwa pale tarehe ya mwisho (deadline) inapokaribia. Deadline inapokaribia, hamasa ya mtu kufanya kazi huongezeka mara dufu. Mtu anapofikiri bado ana muda anakuwa kwenye hatari kubwa sana ya kupoteza hamasa ya kufanya vitu. Ndiyo maana imekuwa rahisi sana kuahirisha na kusema nitafanya kesho. Laini huwezi ukasema utafanya kesho wakati deadline yake ni leo. Ukiamka na kujua kuwa jambo ulilotakiwa kufanya mwisho wake ni leo, ni sawa na kuamsha mtu aliyekuwa kwenye usingizini mzito.
Kumbe umekosa faida hii kubwa ya deadline ambayo ingekusaidia kupiga hatua kubwa maishani mwako. Umekosa fursa hii kwa sababu umeamua kuishi bila malengo na hivyo kuamua kufanya chochote kwa muda wowote ule. Ni ngumu sana kupiga hatua katika mazingira ya uhuru na mazoea kama hayo. Ndiyo maana JimRohn alisema “Without a senseofurgency, desirelosesitsvalue” akimaanisha kuwa bila kuwa na udharura hamasa inapoteza thamani yake. Deadline huibua na kulinda hamasa ya kuchukua hatua za kutimiza mipango.
Ili uweze kutumia faida ya deadline, inakupasa uwe na malengo yako yenye sifa bora. Malengo yenye sifa bora yana deadlines na ili kuweza kuzifikia deadlines hizo malengo yenye sifa hugawanywa kwenye vipande vya mwaka, robo mwaka, mwezi, juma na siku. Hivyo kila siku unakuwa na vitu ambavyo inakupasa uvitimize kabla siku yako haijaisha. Hivyo kila siku inakuwa na dharura kwako kwani una orodha ya mambo ambayo utatakiwa uyafanye na kuyakamilisha. Hivi ndivyo watu waliopiga hatua kubwa wanavyofanya.
Licha ya kuwa na malengo yenye deadline, lakini bado imekuwa shida kwako kupiga hatua. Kuna kitu kimoja muhimu ambacho kinakosekana kilichotakiwa kuambatanishwa na deadline. Mwanafunzi huongeza nguvu, muda na umakini pale deadline ya mtihani inapofika kwa hofu kushindwa au kwa matamanio ya kufaulu. Kampuni huweka jitihada mwisho mwa robo mwaka, ili wawe na ripoti nzuri kwa mamlaka husika kama vile bodi. Kwenye mifano hii miwili utaona kuwa kuna nguvu kubwa ambayo huwa inawasukuma ili waweze kufikia malengo ya deadline. Je wewe kuna kitu gani kinakusukuma kufikia malengo ya deadline?
Licha ya deadline, hakikisha kuna mtu ambaye unawajibika kwake. Ili uweze kupiga hatua kubwa maishani mwako andaa mtu ambaye atakuwa anakusimamia kukamilisha uliyoyapanga. Kama huna mpango huo, ni rahisi sana kutotekeleza licha ya kuwa na deadline kwa sababu ni vigumu kujiadhibu mwenyewe.
Ndugu! Kuna mambo umetamani uyapate maishani mwako, lakini kila ulivyopanga ilishindikana kuyatimiza na ukaishia njiani. Wakati wake wa kuyatimiza umefika. Weka lengo hilo wazi na kuligawa mpaka kipande unachoweza kufanya kwa siku. Kisha tafuta mtu ambaye utakuwa unawajibika kwake ili akusukume kuchukua hatua. Nipo tayari kukusukuma kuchukua hatua kwenye deadlines zako. Kupata huduma hii piga 0752 206 899. Pia unaweza kupakua bure kabisa mwongozo wa kuweka na kutimiza malengo kupitia kiunganishi hiki
https://www.amshauwezo.co.tz/mwongozowamalengo
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz