Kwa Nini Umejitahidi Kuwa ‘Busy’ Sana Lakini Bado Unapata Kiduchu?


Categories :

Ukiamka asubuhi na kuenda mitaani utakutana na watu wengi sana wakitoka nyumbani kwao na kwenda kazini. Baada ya jua kuchwa kadhalika utakutana na watu wakiwa njiani pia wakirudi kwenye makazi yao, huku wakiwa wamechoka kuashiria wametumia nguvu kubwa kufanya kazi. Hiki ni kiashiria tosha kuwa watu wapo ‘busy’ wakifanya kazi.

Wengine wameenda mbali zaidi kwa kuandaa orodha ya majukumu ambayo wanatarajia kuyatimiza kwa siku hiyo. Ikifika jioni orodha hiyo huonekana  na alama ya vema kwenye kila kazi iliyopangwa kufanyika siku hiyo ikiashiria kuwa kazi zote au asilimia kubwa ya kazi zilizopangwa kufanyika zimefanyika. Lakini kumekuwa na mshangao mkubwa  kwa watu wengi kuona licha ya  nguvu na muda wanaouwekeza ni tofauti na matokeo wanayopata. Yaani nguvu na muda unaowekwa ni vikubwa kuliko matokeo wanayoyapata.

Kuwa busy kisha kuishia kupata matokeo kidogo yasiyoridhisha imekuwa sababu moja wapo ya watu kutofurahia kile wanachokifanya kwa kuona wanakipa muda lakini hakiwapi kile wanachotarajia. Hii imekuwa sababu pia ya watu kupata na msongo wa mawazo na kukata tamaa za kuendelea na safari. Zifuatazo ni sababu zinazochangia wewe kuendelea kupata kiduchu ukilinganisha na nguvu na muda unaowekeza;

Kutokuwa na malengo yanayoamsha. Malengo ndiyo dira ya nini unataka kufanya na kupata matokeo tarajiwa. Watu wengi wanakuwa wakiwekeza nguvu na muda wao kwenye matamanio na sio malengo. Tofauti ya malengo na matamanio ni kuwa malengo huwa yanakuwa wazi kabisa wakati matamanio ya kupata kitu huwa ni mawazo fulani yanayoelea hewani. Ni vigumu kupata matokeo yanayoeleweka na kuridhisha kama utakuwa unafanyia kazi matamanio na sio malengo. Ili uweze kuongeza uzalishaji wa kupata matokeo yanayolingana na nguvu na muda unaowekeza huna budi kuwa na malengo yanayokuamsha na yenye sifa bora.

Kupungukiwa na nguvu. Ili uweze kuwa na ufanisi mkubwa na kufanikiwa kuzalisha matokeo bora na makubwa huna budi kuzalisha nguvu pia. Nguvu zinazozungumziwa hapa ni za akili, hisia na mwili kwa ajili ya kufanya kazi. Huwezi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kama utakuwa na huzuni, hasira, kisasi nk. Utakuwa na uzalishaji mkubwa kama  utafanya kazi ukiwa na furaha, upendo amani nk. Mwili utakuwa radhi kuzalisha nguvu na kuzalisha matokeo makubwa ya kazi kama utakuwa na afya imara na pia umeupumzisha baada ya kazi kwa wastani wa masaa saba. Kama mwili, akili na hisia ni dhaifu havitakuwa radhi kuzalisha matokeo unayoyatarajia.

Usumbufu kazini. Unaweza ukasema nilikuwa busy na kazi kwa masaa kumi, lakini kiuhalisia ukawa umefanya kazi masaa matano au pungufu ya hayo. Kumekuwa na usumbufu mwingi sana zama hizi. Simu ya mkononi hasa simu janja, licha ya faida zake nyingi lakini imekuwa na hasara kubwa sana, hasa kwenye usumbufu. Kufanya kazi huku ukiendelea kusoma  jumbe za mitandao ya kijamii au ujumbe mfupi wa simu au ukiwa unaendelea kupokea na kusikiliza simu umekuwa ni usumbufu mkubwa sana ambao umeharibu muda mzuri wa mtu kufanya kazi kwa ufanisi. Je huwa unakumbuka kutoa muda unaopokea simu katikati ya kazi kwenye muda unaohesabu umetumia kwenye kazi? Je huwa unakumbuka kutoa muda unaotumia kuingia kwenye mitandao ya jamii pale unapoona umechoshwa na kazi? Basi hii ni sababu mojawapo ya uzalishaji wako kuwa kiduchu licha ya kujiona upo busy.

Ndugu! Naamini una tamaa ya kuwa na uzalishaji mkubwa kutokana na u-‘busy’ ulionao.  Sababu hizo hapo juu zimekuwa miongoni mwa vizuizi vya wewe kuzalisha matokeo makubwa yenye ubora wa kukufanya upige hatua kubwa zaidi. Anza kwa kuweka malengo kama umekuwa unaishi kwa matamanio. Lakini kama una malengo angalia kama yana sifa bora za kukufikisha unakotaka kufika. Baada ya kuwa na malengo imarisha afya ya mwili, akili na hisia ili ziweze kukupa nguvu kubwa ya kuzalisha matokeo. Mwisho hakikisha unaepuka usumbufu wowote ili uweze kutumia nguvu hizo kwa ufanisi.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *