Ulichonacho Sasa Ndicho Kinachokuzuia Kupata Unachostahili.


Categories :

Kuna mafanikio fulani ambayo umeshayapata mpaka sasa. Unastahili kujipongeza au kupongezwa kwa ajili ya hayo. Lakini ukilinganisha kile ulichokipata na kile ulichostahili, kuna safari ndefu unayotakiwa kupiga. Kuna mazingira ambayo mafanikio ya sasa au vitu vingine ulivyonavyo vimekuwa vikwazo kupata ulichostahili. Umekuwa ukitafuta aliyesababisha kutoyafikia mafanikio yako makubwa uliyostahili, lakini hujapata jibu.

Umebaki kwenye mafanikio ya kawaida kwa sababu ya vitu ulivyonavyo sasa. Una nini mkononi mwako kinachozuia usipokee kitu kingine. Kikombe kilichojaa maji, huwezi tena kujaza maziwa. Kama utataka ujaze maziwa, itakulazimu umwage kwanza maji ili kupata nafasi ya kumimina maziwa.

Kuna vitu ulivyovishikilia na kuving’ang’ania kwa sababu mbalimbali vilivyokufanya uendelee kubaki ulipo ana mara nyingine kurudi nyuma. Hakuna mabadiliko chanya yatakayotokea maishani mwako usipokubali kubadilika au kuviachia vitu hivyo. Vifuatavyo ni vitu ambavyo inabidi ukubali ili uweze kupiga hatua zaidi na kupata mafanikio makubwa zaidi;

Tabia: Kama tabia ulizonazo sasa zinaendelea kukubakisha ulipo, utambue kuwa hizo hazikufai tena, unahitaji kujenga tabia nyingine. Kama umebaki ulipokwa sababu huna mtaji, jiulize kama una tabia ya kuweka akiba kwenye kila kipato unachokipata? Kama hapana basi ndio muda sasa wa kujenga tabia ya kuanza kuweka akiba. Kama unatoka asubuhi kisha kurudi jioni ukiwa umechoka lakini huoni cha maana ulichokifanya, basi jiulize kama una tabia ya kupangilia siku yako au la? Kama huna basi jenga tabia ya kuanza kuipangilia siku yako.

Mafanikio uliyonayo sasa. Mafanikio kidogo uliyonayo sasa yanaweza kuwa sumu kwenye mafanikio makubwa uliyostahili kuyapata. Je umeridhika na kuona umeshafika mbali sana katika safari yako ya mafanikio baada ya kupata ulichonacho sasa? Je umeridhika na mafanikio uliyo nayo sasa baada ya kuona hakuna mtu yoyote anayekuzunguka anayeweza kuyafika pale ulipo sasa. Linganisha mafanikio yako ya sasa na yale uliyostahili kuyapata kisha chukua hatua.

Marafiki wa sasa. Je watu wako wa karibu wanakuhamasisha kuchukua hatua? Je ukikutana na marafiki zako wanakuhamasisha kuchukua jukumu la maisha yenu au wanalalamika muda wote? Kama rafiki zako hawakusaidii kuchukua hatua, utambue hawatakufikisha unakostahili na huna budi kuwaachia.

Maarifa uliyonayo. Je umesoma sana kiasi cha kuona huhitaji tena kujua kitu kingine? Je unaona maarifa mengine ya maisha hayana maana baada ya kupata mengi ya mfumo rasmi wa elimu? Ndugu pale utakaposema unajua kila kitu ujue unajiandaa kuporomoka. Jenga tabia ya kujifunza kila siku.

Kipato cha uhakika. Kipato cha uhakika si lazima kiwe cha kutosha. Je kuna jitihada zozote unazozifanya kuhakikisha unapata vipato zaidi kutoka kwenye kipato cha uhakika? Vipato vya uhakika au kudumu hutoka kwenye ajira ambako ongezeko la vipato hivyo ni dogo sana. Hivyo ili uweze kutengeneza kipato kikubwa unachostahili huna budi kuzalisha zaidi kutokana na kipato chako cha kudumu.

Angalia ulichokishikilia kwa sasa kati hivyo vitano ulivyovisoma hapo juu. Ni kitu/vitu gani vimechangia wewe kuendelea kubakia ulipo kwa muda mrefu? Ni muda sasa wa kuanza kudondosha au kubadili kimoja baada ya kingine ili uweze kupiga hatua zitakazo kufikisha kule unakostahili. Hakuna miujiza yoyote itakayokufanya utoke ulipo usipochukua hatua sahihi sasa. Chukua hatua leo.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *