Ngazi Tayari Unayo, Kwa Nini Hupandi Juu?
Kama upo sehemu na unataka kupanda sehemu ya juu zaidi, unaweza kutumia kifaa kama ngazi kupanda huko. Urefu wa ngazi ndiyo unaweza kuamua wapi ufike.
Kama ukimuona mtu yupo chini na analalamika kuwa anashindwa kupanda juu wakati ngazi ipo pembeni yake, ungemshangaa sana. Yamkini na wewe ungemlaumu sana na kumuambia huyu mtu hajiongezi au anajipunja mwenyewe.
Lakini na wewe ni kama huyo mtu mwenye ngazi lakini akishindwa kupanda juu. Unaweza ukajiuliza ngazi iko wapi? Ngazi ni vile vitu ambavyo tayari unavyo na vingeweza kukusaidia kupiga hatua zaidi za maisha kuliko hapo ulipofika. Lakini kwa kutovitumia umeendelea kubaki kwenye ngazi ya chini badala ya kupanda juu. Vifuatavyo ni vitu ambavyo tayari unavyo , unavyoweza kutumia kama ngazi kufika mbali;
Maarifa. Kuna maarifa mengi ambayo umejifunza kwa kusoma vitabu au kupitia elimu darasa ambayo ukitumia, yatakutoa hapo ulipo na kukupeleka sehemu ya juu kabisa. Kama umejifunza kuwa ili uweze kufikia uhuru wa kifedha ni lazima uweke akiba. Je kwa nini hutumii maarifa hayo na kupiga hatua. Kama una ujuzi wa kutengeneza bidhaa kama sabuni, fanicha nk kwa nini huanzi kutengeneza? Wewe ni mpishi mzuri sana, kwa ni huanzi kuitumia fani hiyo kuingiza kipato?
Kipaji. Kuna vitu unaweza kufanya kirahisi na kwa viwango vya juu kabisa kuliko watu wengine. Je unatumiaje kipaji hicho kuboresha maisha yako? Una kipaji cha ushawishi ndani yako, kwa nini hutumii kupata wateja zaidi wa biashara yako au mtu mwingine? Unaweza kuimba, watu wanakusifia kuwa una kipaji hicho, umechukua hatua gani kukikuza na kikakuingizia kipato?
Vitu ambavyo huvitumii. Nyumbani kwako kuna vitu umevinunua na kuviweka tu bila ya kuvitumia au kuvitumia kwa kiasi kigogo sana. Kama bado unahangaika mtaji, kwa nini usiviuze hivyo vitu ili upate mtaji wa kuanzisha biashara? Una jokofu ambalo unatumia robo tu ya nafasi yake, kwa nini usilitumie kuweka na kuuza vinywaji vya baridi kwa majirani? Una jiko la kuokea mikate lakini unatumia mara moja tu kwa wiki au mwezi, kwa nini usichukue oda za kuoka mikate ya watu au ukatumia kuaka mikate mingi na kuiuza?
Mafanikio yako ya sasa. Mafanikio yako ya sasa yanaweza kuwa sumu ya kupiga hatua. Watu wengi huridhika na kubweteka baada ya kupata mafanikio fulani. Huona wameshafika mbali kiasi cha kutokuhitaji tena kuongeza jitihada. Kwa kufanya hivyo wamejichimbia kaburi la kuzikwa wenyewe. Angalia mafanikio uliyoyapata na ona nafasi ya kutumia mafanikio hayo kupiga hatua kubwa zaidi. Kama hukui unakufa, hakikisha upo kwenye mwendo muda wote.
Thamani. Kuna nafasi ya kuongeza thamani unayoitoa sasa na kupata kipato zaidi. Mteja unayemhudumia sasa una nafasi ya kumpa thamani zaidi kwa kumuelezea zaidi kuhusu umuhimu wa bidhaa anayoitumia. Una nafasi ya kuboresha huduma unayoitoa. Anza leo.
Ndugu! Sasa utakuwa umeona jinsi ngazi ilivyo karibu nawe lakini umeshindwa kuitumia kupanda juu zaidi. Una vitu vingi sana ndani yako aua vinavyokuzunguka unavyoweza kutumia kama ngazi ya kupandia juu. Je ni maarifa ua ujuzi uliopo ndani yako? Je ni vitu vilivyopo nyumbani mwako unavyoweza kuviuza na kupata fedha za mtaji? Je kipaji chako umeshaanza kukitumia ili kukupa kipato. Angalia ngazi mojawapo iliyo karibu na wewe kisha weka kwa ajili ya kupandia juu.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz