Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukivuta Kitu Kinachoonekana Kuwa Mbali Na Kukiweka Mikononi Mwako.


Categories :

Kila mtu ana vitu anavyovitamani kuwa navyo maishani mwake. Vitu hivyo ni vya kila eneo la maisha yake. Licha ya tamaa hiyo lakini watu wengi wameishia kutamani bila kufanikiwa kuvipata katika maisha yao.  Lakini wapo wachache ambao huwa wanafanikiwa kuvipata vitu hivyo. Nini huwa wanafanya ili kupata vitu wanavyovipenda? Leo utaenda kuifahamu siri mojawapo wanayotumia kuvipata vile wanavyovitaka maishani mwao.

Siri hiyo wanayoitumia wale wanaofanikiwa kuvipata vitu vile wanavyovitaka ambayo na wewe unaweza kuitumia ni IMANI. Hii ni siri inayowawezesha kuvuta hata vitu vinavyoonekana kuwa mbali na kuviweka mikononi mwao. Imani ni kuwa na uhakika wa kukipata kitu hata kabla ya kukiona. Hata pale mazingira yanapoonekana kuwa hayapo upande wako, imani huendelea kuona vitu unavyovitaka vikiwa mkononi mwako.

Kwa kupitia imani unafanikiwa kufika mwisho ungali mwanzoni, yaani unayaona matokeo kwenye fikra zako hata kabla hayajatokea katika uhalisia. Kwa sababu ya ugumu wa maisha, hii ni tabia muhimu sana kwenye kupata chochote unachokitaka. Huwezi kusimama imara ukiendelea na safari ngumu kama hujui ni wapi unakoelekea. Kama hujui unakoelea na kuamini kuwa umeshafika ni rahisi sana kuahirisha safari yako pale unapokutana na vikwazo njiani.

Ili uweze kupata kile unachokitaka, lazima ufikie hatua ambayo utakuwa unakiona kitu unachokitafuta katika picha kamili. Hii ni hatua ya kukimiliki kitu hata kabla ya kukiona. Watu wengi walioshindwa ni wale ambao walikuwa hawauoni mwisho tangu mwanzoni, wanafanya ili kupata chochote na kiasi chochote, ndiyo maana hata baada ya kushindwa hawakushituka kwa sababu walikuwa hawayatarajii. Hivi ndivyo unavyoweza kujenga imani na kukivuta chochote na kuwa mikononi mwako.

Chanzo cha kitu unachokita. Kama kitu unachokitaka kinatoka ndani mwako ni rahisi sana kuamini kuwa ni chako na unaweza kukipata. Kitu kinachotoka ndani yako kinaweza kuwa kinahusu sababu ya wewe kuwepo hapa duniani au ndoto yako unayotarajia kuitimiza. Kitu cha kuambiwa na mtu mwingine ni vigumu kukijengea imani na kuona kitakuwa chako. Je hayo uliyopanga kuyatekeleza yametoka wapi? Ndani yako au kwa mtu mwingine?

Kufanikiwa kupata matokeo ya awali hata kama ni madogo. Hata kitu kikubwa ambacho picha yake unaiona mbeleni hutengenezwa na matokeo madogo madogo. Kwenye kitu kile unachotaka ukipate, anza kukifanya na kufanikiwa kupata matokeo madogo, hii itakusaidia kuamini kuwa hata makubwa yanakuja. Matone machache yanavyodondoka ardhini huongeza imani ya kuwa mvua itanyesha.

Pata uzoefu kwa waliofanikiwa. Ili uweze kupata mafanikio makubwa huna budi kutowachukia wale waliofanikiwa. Hawa ni watu muhimu sana kwako. Kwa kuwapenda na kujifunza kwao namna walivyopata mafanikio, itakupa imani ya kuwa na wewe unaweza kuyapata mafanikio makubwa hata kama hayafanani.

Kiweke karibu na wewe kitu hicho. Ili kitu kiwe chako lazima kiwe sehemu ya maisha yako. Kitu chochote unachokitaka lazima akili yako ikitambue na akili yako itawaliwe. Weka mazingira ya kuhakikisha unakikumbuka na kukihisi wakati wote.  Kipe muda wa kukifikiri, kukiandika na kukisema. Kama unataka fedha kiasi fulani, basi fikiri kiasi hicho kila wakati, pia kihisi kwa kuona tayari kipo mikononi mwako.

Imani ina nguvu kubwa ya kukuwezesha kukipata kitu hata kile kinachoonekana kipo mbali sana. Huna budi kutengeneza mazingira ya kuona kile unachokitaka kipo mikononi mwako. Ukifanikiwa kutengeneza mazingira hayo, yatakupa ujasiri wa kuanza na kuendelea kukitafuta kile unachokitaka bila kujali changamoto unazokutana nazo.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *