Jinsi Ya Kupanda Juu Ya Vikwazo  Vya Mafanikio Yako.


Categories :

Ndege ikisharuka, rubani huhakikisha anaipaisha juu zaidi kutoka ushawa wa bahari kabla ya kuiacha kukaa kwenye usawa huo. Unaweza ukajiuliza kwa nini rubani huwa anakimbia kimo kifupi kutoka kwenye usawa wa ardhi? Rubani huikimbiza ndege hiyo kutoka kwenye vikwazo vingi ambavyo vipo kwenye kimo kifupi kutoka ardhini. Vikwazo hivyo ni kama upepo mkali na mawimbi ambayo huiyumbisha ndege na kuiweka ndege kwenye hatari kubwa kiusalama.

Maisha yako pia ya kujenga mafanikio yana vikwazo vingi sana kabla ya kufikia mafanikio hayo. Ili uweze kupata mafanikio hayo huna budi kuhakikisha unakaa juu ya kila kikwazo kinachosimama mbele ya njia ya kupandia mafanikio yako. Wanaofanikiwa si kwamba wao hawakutani na changamoto, la hasha! wanakutana na changamoto kama ilivyo kwako, lakini hufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanakuwa juu ya changamoto hizo badala ya changamoto hizo kupanda juu yao na kuwatawala. Na wewe unaweza kujenga uwezo wa kupanda juu ya changamoto na kupata unachotaka kama ifuatavyo;

Endelea huku ukijifunza na kuboresha. Moja ya kitu ambacho walioshindwa huwa wanafanya wanapokutana na changamoto za mafanikio ni kuacha kile wanachofanya na kurudi nyuma. Huu huwa unakuwa mwisho rahisi kwao. Huwezi kufika popote kama utaacha kufanya kile unaamini kitakufikisha kwenye mafanikio pale unapokutana na changamoto. Ukikutana na changamoto huna budi kuendelea na kile unachokifanya huku ukijifunza kwa haraka na kurekebisha makosa unayoyafanya.

Fanya kwa umakini mkubwa kile unachokifahamu. Unapoanza na kuendelea na safari ya kusaka maisha, kuna vitu unavijua vizuri na unaweza kuvifanya kwa ubora mkubwa. Huko ndiko inabidi uwekeze nguvu zako na kufanya kwa ubora mkubwa ili kutoa thamani kubwa na kupata matokeo makubwa huku ukiendelea kufanyia kazi maeneo uliyo dhaifu taratibu.

Jenga imani huku ukitenda. Ili uweze kutoka chini ya vikwazo vingi vya mafanikio na kupanda juu yake lazima uwe na imani kuwa vile unavyovifanya ndivyo vitakavyokupa matokeo mazuri. Imani itakusaidia kuvuka milima ya changamoto. Hata pale ambapo utaweka nguvu lakini huyapati matokeo utaamini kuwa yanachelewa tu, lakini yatakuja. Amini kuwa matokeo yatakuja huku ukiendelea kuweka nguvu kutoka pale unapokwamishwa.

Kaa na watu wanaokuhamasisha. Kazi ya kutoka chini kwenye vikwazo kisha kupaa juu kupata matokeo ni kazi ngumu sana inayohitaji hamasa kubwa ili kusonga mbele. Hivyo ni muhimu kuzungukwa na watu ambao watakutia hamasa hata pale utakapokuwa unakutana na magumu. Kwa mfano ukizungukwa na watu waliokwisha kufanikiwa katika yale unayopitia wewe inakuwa rahisi kukuhamasisha na wewe kuhamasika kwa kuona unachotaka kuifanya kinawezekana.

Kushindwa kusiwe chaguo lako. Kwenye jambo lolote unalolifanya kuna machaguo mawili unayoweza kuyachagua; kushinda au kushindwa. Una uweo wa kuamua kuendelea kukitafuta kitu kwa gharama yoyote ile mpaka ukipate. Huu ni uamuzi mzuri lakini wenye kuwajibika. Watu wanaofanikiwa huamua hivyo, kuwa wataendelea kukitafuta kitu wanachokitaka mpaka wa kipate au watakufa wakiwa wanakitafuta.  Ili uweze kuwa juu ya vikwazo vyovyote vile kushindwa kusiwe chaguo lako bali kushinda.

 Hivi ndivyo unavyoweza kupanda juu ya vikwazo na sio vikwazo kupanda juu yako na kushindwa kupata kile unachotaka. Ukishaamua nini unataka weka msimamo kuwa utaendelea kukitafuta kitu hicho huku ukiweka kila ulichonacho kuhakikisha utakipata unachotaka, hapo ndipo vikwazo vitakapokupisha upande juu.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *