Utajiri Wowote Unaanza Kwa Kuwekeza Kwanza Hapa.
Maisha ya mwanadamu yamejaa mahangaiko ambayo mengi hulenga kupata utajiri. Watu wengi wakisikia neno utajiri hufikiri uwingi wa fedha tu, lakini neno hili lina maana zaidi ya uwingi wa fedha. Utajiri ina maana ya kuwa na utele kwenye vitu unavyovitaka, viwe vile vinavyoonekana na hata visivyoonekana. Ni tamaa ya mtu kuwa na utajiri wa fedha au mali, utajiri wa mahusiano, umaarufu nk. Utajiri wa fedha au mali umeshika nafasi kwa sababu matatizo mengi yanayokusumbua yanaweza kutatuliwa kwa kuwa na fedha.
Licha ya tamaa kubwa na mahangaiko ambayo watu huwa wanakuwa nayo kwa sababu ya kupata utajiri, lakini bado watu wengi wanashindwa kupata utajiri huo. Kuna watu wengi wamefikiwa na umauti hali wakiendelea kutafuta utajiri. Kuna watu waliozeeka na kuona hawana nguvu tena za kuendelea kutafuata utajiri huo. Kwa nini watu hawaupati utajiri huo licha ya jitihada hizo wanazoziweka?
Miongoni mwa sababu kuu zinazosababishwa watu kutopata utajiri ni kutoanza kuwekeza sehemu sahihi. Utajiri ni matokeo, na kulingana na sheria ya kisababishi na matokeo, huwezi kupata matokeo mpaka uweke visababishi. Kuweka visababishi ni kuwekeza. Wapi unaanza kuwekeza, ndipo tatizo la watu kutopata utajiri linapoanzia. Watu wengi wamekuwa wakihangaika kuwekeza utajiri wao nje kabla ya kufanya hivyo ndani mwao. Utajiri wowote unaanza kawa kuwekeza kwanza ndani yako.
Chochote utakachokifanya au kitakachotokea katika maisha yako lazima kiwe kimekaa na kukua kwenye akili yako ya ndani. Kwa mfano kama unataka kupata utajiri wa fedha wa bilioni mia moja, ni lazima utajiri huo ujengeke kwanza ndani yako kiasi cha akili yako kuamini kuwa tayari kiasi hicho kipo mikononi mwako licha ya kuwa bado kukufikia. Uwekezaji huu wa ndani unafanywa kwa mawazo yaliyoambatana na imani.
Ndiyo maana Napoleon Hill alisema kuwa ‘’chochote ambacho akili itakipokea na kukiamini itakipata’’ Kumbe mahangaiko ya kuupata utajiri inabidi yaanzie kwenye akili na si vinginevyo. Inakupasa ukazane kwanza kuiaminisha akili yako mpaka iamini kuwa utajiri unaoutaka unaweza kuupata ndipo uendelee na uwekezaji wa nje.
Akili yako ya nje (conscious mind) inaathiri kubwa sana kwenye uwekezaji wa utajiri wako kwenye akili ya ndani. Kile unachokisema, waza na kukiongea mara kwa mara na kukiamini ndicho kinachoenda kuzama ndani yako kukupa matokeo. Hivyo kama akili yako ya nje itaendelea kuongea maneno ya umasikini, kuwaza mawazo ya umasikini na kuamini umasikini basi tambua unafanya uwekezaji wa umasikini kwenye akili ya ndani. Hivyo kuanzia sasa hakikisha unachunga sana vitu vyote vinavyofanywa na akili yako ya nje.
Uwekezaji wa utajiri kwenye akili yako ya ndani unafanyika kwa kuipelekea akili hiyo mawazo yaliyoambatana na imani mara nyingi iwezekanavyo. Unataka utajiri gani kwenye maisha yako. Kumbe jambo la kwanza ambalo unatakiwa kulifanya wakati wa uwekezaji wa ndani mwako ni kutambua kwa dhati utajiri unaoutaka, kisha sema maneno haya mara kwa mara huku ukiweka imani kwenye maneno hayo. Haya ni maneno unayoweza kuyasema kwa akili ya nje kisha ya kazama kwenye akili ya ndani; mimi ni bilionea, nina marafiki wema, mimi ni baba au mama mwema wa mfano, najikubali mwenyewe, nina uwezo mkubwa ndani yangu, mimi ni mshindi nk.
Ili mawazo haya yaweze kuzama vizuri kwenye akili ya ndani na kuweza kuzaa matunda ya utajiri huna budi kuyarudia kusema mara kwa mara kwa hisia na imani. Chukua hatua leo ya kuanza kutengeneza utajiri wa ndani. Chagua mawazo ya utajiri kwenye kila eneo la maisha yako kisha yaumbie maneno ambayo utaanza kuyatamka kwa hisia na imani kwa dakika tano mara tatu kwa siku.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz