Hivi Ndiyo Vizuizi Vinne Ulivyoviruhusu Vikuzuie Kupata Mafanikio, Viondoe Leo.
Kama safari za magari zilivyo na vikwazo vingi barabarani, vivo hivyo kwenye safari za mafanikio. Hakuna safari ya mafanikio iliyo rahisi. Safari hizi zina mabonde na milima mingi ya kupanda. Hii ni sababu mojawapo inawafanya watu wengi wasiyapate mafanikio hayo licha ya kuyatamani.
Asilimia kubwa ya vikwazo vinavyosimama kwenye barabara ya mafanikio yako vinatoka ndani yako. Yaani wewe ndiye mhusika mkubwa wa kukwamisha mafanikio yako. Ukiukagua mwili wako utashindwa kuviona kwani vingi havionekani kwa macho. Kama mafanikio yanavyochangiwa na asilimia kubwa ya vitu visivyoonekana vivo hivyo hata kushindwa kunasababishwa na vitu visivyoonekana.
Kuna faida kubwa ya vikwazo hivi vingi vinavyosababisha usifanikiwe kuwa ndani yako. Faida hiyo ni kuwa ukitambua wewe ndiwe mchawi mkuu wa mafanikio yako inakuwa rahisi kuchukua jukumu la kubadilika ili uweze kubadili matokeo na kupata mafanikio. Mara nyingi umekuwa ukitafuta ni nani mchawi wa mafanikio yako! Mara nyingine umeona kuwa serikali ndiyo kikwazo kikubwa cha mafanikio yako. Umekuwa ukiona matajiri pia ndiyo wanaosababisha wewe kuwa masikini kwa wao kuchukua fedha zote. Umeenda mbali zaidi na kuona biashara ya jirani yako ndiyo kikwazo cha wewe kutofanikiwa, lakini vifuatavyo ni vikwazo ambavyo vimesababisha wewe kuwa hapo ulipo;
Kuahirisha mambo. Hiki ni kikwazo kikubwa sana cha kuyapata mafanikio yako. Hujafika hapo kwa sababu ya kutokujua nini ufanye bali kwa kutochukua hatua kwa kitu sahihi ulichotakiwa ukifanye. Nitafanya baadaye au kesho imesababisha watu wengi kutoishi maisha yao waliyostahili. Kwa sababu ya ugumu wa safari hii ya kutengeneza mafanikio makubwa , watu wengi wamejifariji kwa kusema watafanya baadaye pale wanapokutana na ugumu. Kila wakati kuna kesho au baadaye nyingine hivyo baadaye au kesho haitafika. Kuanza kupata matokeo unayotarajia anza kuchukua hatua za mipango mizuri uliyoweka, na wakati sahihi wa kufanya hivyo ni sasa.
Kuwaiga/kuwasikiliza watu wengine. Umeshindwa kuchukua hatua ua umepiga hatua chachekwa sababu ya kuwasikiliza watu kwenye kile unachokifanya. Mara ngapi umekuwa na wazo zuri kutoka ndani yako la kufanya kitu fulani lakini ukaamua kusikiliza maoni ya watu kwanza? Je ulipomshirikisha mtu mwingine hakukukatisha tamaa kwa kuambia hicho unachokiwaza hakiwezekani, kwa sababu katika maisha yake hajawahi kumuona mtu akifanikiwa katika hilo? Hakuna jambo kubwa unaloweza kulifanya kama utasubiri maoni ya watu. Ukishasikiliza sauti ya ndani mwako kwamba inabidi ufanye kitu fulani, basi anza kuchukua hatua bila kujali maoni ya watu wengine.
Kusema ndiyo kwenye kila jambo. Safari ya mafanikio yako huhitaji muda wa kutosha ili kufika mwisho. Hata kabla hujaanza safari unaweza kukutana na vitu vingine vingi tu vitakavyohitaji muda wako. Kwa sababu umekuwa ukisema ndiyo kwenye kila jambo, umetengeneza kikwazo cha kukuzuia kupiga hatua. Wakati umefika wa kuwa bahili kwenye muda wako. Kabla hujasema ndiyo aangalia ni kwa namna gani jambo unalolipa muda wako litakuwa na mchango kwenye mafanikio yako.
Mitandao ya kijamii. Moja ya hitaji muhimu sana katika mbio ndefu za kuyapata mafanikio makubwa ni umakini. Hii ni kuielekeza akili yako na hisia zako kwenye kitu unachokifanya. Unakuwa kile unachokiwaza kwa muda mrefu. Katika zama hizi za teknolojia, umakini wa watu wengi umeibwa sana na mitandao ya kijamii kama vile wasap, facebook, instagram nk. Hivi ni vitu ambavyo ufuatiliaji wake umechukua umakini mkubwa wa watu. Umakini na muda unaouwekeza kwenye mitandao ya kijamii imekuwa kikwazo kikubwa cha kufikia mafanikio yako. Kuanzia leo hakikisha mitandao ya kijamii haiwi kikwaazo tena katika safari ya mafanikio yako. Tenga muda maalumu na mchache wa kutumia kwenye mitandao hiyo na hakikisha matumizi yake hayanyang’anyi umakini wako.
Ndugu, hivi ni vikwazo ambavyo vipo ndani yako vinavyokukwamisha kupiga hatua. Lakini una faida ya kuanza kukiondoa kimoja baada ya kingine kwa sababu vipo ndani yako na vinahitaji tu uamuzi wako na kujitoa kwako. Unaanza kukitoa kipi leo?
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz