Huyu Ndiye Mtu Sahihi Wa Kujilinganisha Naye Ili Uweze Kupiga Hatua Kamili.


Categories :


Ni hulka ya watu kujilinganisha kujua kama anapiga hatua au la. Kuna faida kubwa ya kujilinganisha kwani ndipo unapoweza kujua ulipofika na unakotakiwa kufika. Licha ya faida hiyo lakini kuna changamoto kubwa ya unajilinganisha na nani?

Ulinganisho unakuwa na faida pale tu unapojilinganisha na mtu sahihi. Ukijilinganisha na mtu sahihi utajua kwa dhati ni wapi ilibidi ufike na sasa uko wapi? Ukijilinganisha na mtu huyo utajua uwezo wako wa ndani na kutambua nafasi ya kuweza kuutumia kikamilifu.


Mtu sahihi wa kujilinganisha naye ni wewe mwenyewe. Hiki ndicho kipimo sahihi cha kujilinganisha na si vinginevyo. Kuna watu wamejilinganisha na majirani na kuona kipimo hicho ni sahihi na kuwa wapo bora kuliko hao na kisha kubweteka. Wapo wanaojilinganisha watu waliotangulia kimafanikio wakaona wakifika viwango vile watakuwa wamefika mbali sana. Lakini kipimo sahihi cha kujilinganisha ni wewe mwenyewe.

Kutokujilinganisha kiusahihi kumesababisha watu wengi kutopata mafanikio waliyostahili. Kwa mfano kama imezungukwa na wa jamii ambayo haijapiga hatua kubwa na kupata mafanikio makubwa ni rahisi sana kujiona wewe ni bora sana kuliko wanaokuzunguka pale utakapopata mfano hata kama madogo. Utambuzi utakaokuwa unaupata kwa watu wa kuwa umepiga hatua kubwa unaweza kukulewesha na kuhisi umeshafika kileleni na huna haja kuendelea kupanda zaidi. Hivyo ulinganisho sahihi ni ule unaojilinganisha na wewe mwenyewe. Zifuatazo ni sababu za kwa nini ujilinganishe na wewe mwenyewe na kile kinachokwenda kutokea;

Kiwango chako sahihi kipo ndani yako. Kila binadamu ana uwezo wake wa kipekee ambao huwezi kuulinganisha na mtu mwingine. Kujilinganisha na mtu mwingine ni kujidanganya kwani ni vitu viwili tofauti.

Kila mtu ana kazi tofauti. Upo duniani kwa sababu maalumu, unapojilinganisha na wewe unakuwa unajilinganisha na kazi sahihi uliyopo nayo. Kujilinganisha na mtu mwingine ni kulinganisha kazi mbili tofauti ambazo haziwezi kulinganishwa na kujua kuwa umefanya kwa viwango sahihi.

Ukijilinganisha na wewe mwenyewe unapata ridhiko la moyo. Ukifanikiwa kujilinganisha na wewe mwenyewe na kuishi kile kiwango cha kweli cha kutoka ndani yako, utafikia kiwango cha juu sana unachostahili. Hiki ni kiwango ambacho kitakupa ridhiko kuliko ungejilinganisha na mtu mwingine.

Ukijilinganisha na wewe mwenyewe hujipunji. Si rahisi kufikia kiwango timilifu kama utajaribu kujilinganisha na mtu mwingine. Kwa sababu huna zana za kuwa kama mtu huyo, utaishia kufanya chini ya kiwango. Una zana maalumu kwa ajili ya kazi maalumu, unapojilinganisha na wewe mwenyewe unawianisha na zana kamili ulizonazo na kiasi unachopaswa kukipata kama utazitumia vizuri. Hivyo inakuwa sio rahisi kupunjwa.

Ndugu umefika hapo ulipo kwa sababu ya kulinganisha safari yako na safari ya watu wengine, ndiyo maana hujafika maili zinazotakiwa. Umepata mafanikio kiduchu kwa sababu ya kuona wewe ni bora kuliko watu wengine unaojilinganisha nao ambao nao hawajaishi viwango vyao halisi. Una hatari kubwa ya kufa na uwezo wako kabla hujautumia kwa sababu ya kujilinganisha na watu wengine.

Ndugu! Una uwezo wa kufanya mambo makubwa na miujiza kama utaangalia ndani yako kile ulichonacho na kufanya bidii kifikia kiasi ambacho ulistahili. Kuanzia sasa acha kujilinganisha na mtu mwingine yoyote kwani hakuna mtu mwingine kama wewe wa kujilinganisha naye kwa usahihi.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *