Ifahamu Tabia Hii Itakayokupa Matokeo Makubwa Maishani Mwako.
Maisha ya mwanadamu yanajengwa na tabia. Tabia za mwanadamu ndizo huamua nini akifanye na asikifanye maishani mwake. Licha ya utofauti wa rangi, umri au kabila, binadamu hutofautiana kitabia.
Tofauti kubwa pia kati ya watu waliofanikiwa na walioshindwa huwa kwenye tabia. Watu waliofanikiwa wana tabia fulani ambazo watu walioshindwa hawana na kwa kuziishi tabia hizo wanafanikiwa kupata mafanikio ambayo walioshindwa hawayapati. Kadhalika walioshindwa wana tabia pia ambazo wanaziishi tofauti na wale waliofanikiwa, kwa kuziishi tabia hizo hizo wanashindwa kupata au wanapata mafanikio kidogo ukilinganisha na wale waliofanikiwa. Hivyo kuna tabia za kufanikiwa na tabia za kushindwa. Tabia utakazozijenga na kuziishi ndizo zitaamua nini ukipate maishani mwako.
E.M. Gray alitumia muda mwingi wa maisha yake kutafiti kuhusu kigawe kikuu cha mafanikio. Baada ya kuwatafiti watu wengi waliofanikiwa, alitambua kuwa licha ya bidii ya kazi, bahati, mahusiano mazuri, na sababu nyingine lakini kuna na tabia nyingine ilipatikana kwa kila mwanamafanikio. Tabia hiyo “kufanya vitu ambavyo walioshindwa hawapendi kufanya”. Stephen Covey aliita tabia hii kuweka vitu vya kwanza, kwanza.
Maisha ya mwanadamu yamezungukwa na vitu vingi ambavyo anaweza kuvifanya kupitia tabia zake. Lakini vitu ambavyo vinampekela mtu kwenye mafanikio makubwa havipendwi kufanywa na hii ndiyo inayopelekea watu wachache tu duniani kufanikiwa. Waliofanikiwa wanaitambua siri hii ndiyo maana licha ya ugumu wa kufanywa vitu ambavyo walioshindwa havifanyi wao hujitoa kuvifanya hivyo na ndivyo vilivyowapa mafanikio hayo makubwa na ya utofauti.
Kwa mfano ili uweze kufanikiwa kwenye biashara yako lazima ufanye mauzo yatakayokupa faida na kuikuza biashara yako. Moja ya changamoto kubwa katika mauzo ni kukataliwa na watu wakati wa kufanya mauzo. Walioshindwa hujizuia kuuza bidhaa au huduma zao kwa watu ambao hawajawazoea kwa kuogopa kukataliwa na hivyo kushindwa kukuza mauzo, faida na biashara zao. Hapa ndipo waliofanikiwa huja kutofautiana na walioshindwa, wao ndio hujitoa kuwauzia hata watu wale wasiowazoea na bila ya kujali kama watakataliwa au la. Kwa kufanya hivyo wanapata nafasi ya kuuza sana, kupata faida kubwa kisha kukuza biashara zao sana.
Ili uweze kujenga tabia hii kuweka vitu vya kwanza kwanza huna budi kujitoa kweli kutoka ndani mwako. Tabia utakayotaka kuijenga lazima iwe na shauku kubwa ya ndiyo kuliko hapana la sivyo inakuwa rahisi kurudi nyuma. Kitu ambacho unataka kufanya kwa mazingira yoyote yale lazima kiwe tayari kimejengeka kwenye akili yako na kuna faida kubwa sana ya kujilazimisha kufanya licha ukinzani utakaokutana nao. Sababu ya kufanya lazima iwe kubwa ya kukufanya utengeneze tabia nyingine nje ya mazoea.
Chagua leo kitu kimoja kwenye eneo la maisha yako binafsi na kimoja kwenye maisha ya taaluma yako au biashara ambavyo unaona ukivifanya kila siku au wakati vitaleta matokeo makubwa chanya katika maisha yako. Je unachagua kusoma kitabu kimoja kila mwezi au wiki na kuweka kwenye vitendo angalau kitu kimoja ulichojifunza? Je kwenye biashara yako unachagua kutafuta wateja kumi wapya wa bidhaa zako au huduma yako bila kujali ukinzani utakaoupata?
Ndugu! Hii ndiyo nafasi pekee ya kuanza kutengeneza tabia ambayo italeta matokeo makubwa maishani mwako. Kaa chini na tafakari ni jambo ulilo na shauku kubwa ya kulipata maishani, kisha lijengee tabia ya kulifanya hata pale utakapokuwa hupendi kufanya. Hii ndiyo tabia pekee ambayo kila aliyefanya makubwa nayo, na wewe ijenge na kuiishi.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz