Hiki Ndiyo Kitu Pekee Cha Kufanya Pale Unapotaka Matokeo Tofauti.


Categories :


Nitafanya nini sasa? Mh! Mbona mambo hayaendi? Kuna njia nyingine naweza kufanya? Haya ni maswali ambayo umekuwa ukijiuliza mara nyingi sana. Inawezekana pia hata sasa unajiuliza maswali hayo pia. Inawezekana umechukua uamuzi wa kukata tamaa baada ya kukosa majibu ya maswali haya.

Kuna kitu sahihi unachoweza kukifanya katika hali hii. Mpaka kufikia kukwama inamaanisha kuna vitu ulikuwa unavifanya, lakini kwa sasa havikupi matokeo unayotaka. Siri ya kupata matokeo tofauti imejificha kwenye miongoni mwa kanuni za asili inayosema kwenye kila matokeo unayoyapata kuna visababishi.


Hivyo kama kuna matokeo unayoyapata sasa hata yale ya kukwama, tambua kuwa kuna vitu ulivyovifanya kukupelekea kufanya. Kumbe kama unataka kupata matokeo tofauti, inakupasa uweke visababishi vingine. Kumbe kitu pekee unachotakiwa kufanya pale unapotaka matokeo tofauti ni kufanya kinyume na unavyofanya sasa.

Kufanya kinyume na sasa ni kuweka visababishi tofauti na vya sasa, iwe kwa kiasi au aina ambavyo kutokana na sheria vitakupa matokeo tofauti.

Kama una kipato kidogo ina maanisha unatoa thamani ndogo kwa sababu ya kuwa na mifereji michache ya kipato au mifereji uliyonayo inafanya chini ya kiwango. Kama hapa ndipo ulipokwama, fanya kinyume chake ili upate matokeo tofauti yaani kipato kikubwa. Ongeza thamani kwa kuboresha unachokifanya sasa au ongeza mifereji zaidi ya kukuingizia kipato.

Kama maisha yako ya sasa ni ya huzuni, ina maana kuna visababishi vilivyoleta hali hiyo. Je ni kwa sababu sio mwepesi wa kusamehe bali ni wa kulipa visasi? Je unawaza mawazo hasi kila wakati? Je unafikiri furaha imejificha kwenye vitu au matokeo na sio kwenye uhai wako? Katika mazingira kama hayo utapata matokeo ya utofauti kwa kuweka visababishi tofauti na unavyoviweka sasa ili upate matokeo tofauti ambayo ni furaha. Badala ya kulipa visasi wewe toa msamaha. Badala ya kuikaribisha mawazo hasi wewe karibisha chanya. Badala ya kusubiri mpaka upate kitu fulani ndio ufurahi, wewe furahi angali upo hai.

Kama umefanya mambo mengi na kuona umepata vingi lakini huhisi kuridhika, ujue ulivyovifanya ndiyo vilivyokufikisha hapo. Hii inamaanisha kuwa umefanya vitu vingi vizuri lakini bado hujafanya kazi yako kikamilifu. Yamkini unajiuliza, kazi ipi tena? Kuna kazi maalumu uliyoletewa hapa duniani uifanye, kazi hiyo kusudi la maisha yako. Hapa ndipo unapohitaji kisababishi cha ridhiko la maisha yako ambacho ni kutambua na kuishi kusudi lako kikamilifu.

Kama biashara yako haikui na haitoi faida kiasi cha kutaka kufa, fahamu kuwa kuna visababishi vilivyokufikisha kwenye matokeo unayoyapata sasa. Je ni thamani gani unawapa wateja wako? Je unampa mteja thamani kubwa kiasi cha kuona hana haja ya kwenda sehemu nyingine anapokuwa na uhitaji wa bidhaa aua huduma unayoitoa? Je gharama za uendeshaji ni kubwa kuliko faida unayotengeneza? Kama hayo ndiyo yanayosababisha biashara yako kutaka kufa, basi huna budi kuweka visababishi tofauti. Anza kuongeza na kuwa na wateja wa kudumu wa biashara yako. Hakikisha gharama za uzalishaji ni ndogo kuliko faida unayotengeneza.

Ndugu! Pale unapotaka matokeo tofauti, jambo la kwanza unalotakiwa kutambua ni kuwa unahitaji visababishi tofauti na vile vinavyokupa matokeo ya sasa ambayo huyapendi. Mara zote visababishi hivyo huwa ni kinyume na vile vya sasa.

Ni hali gani unayoipitia sasa na unawiwa kuibadilisha? Anza na kuangalia kile ulichokifanya mpaka kufika hapo kisha fanya kinyume na yale yaliyosababisha ili kupata matokeo unayoyataka sasa.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

1 thought on “Hiki Ndiyo Kitu Pekee Cha Kufanya Pale Unapotaka Matokeo Tofauti.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *