Mtoto Anayelia Sana Ndiye Anayenyonyeshwa.
Mbinu kuu anayotumia mtoto kueleza nini anachojisikia au anachokitaka ni kulia. Hata wakati wa kuzaliwa, ili aonekane amezaliwa kawaida inampasa alie, na asipo lia kwa hiari hulazimishwa kulia. Mtoto anapolia mama au mlezi hujua mtoto ana jambo ambalo linamsibu na hana budi kumchunguza au kujua ni nini anakitaka ile apewe.
Kuna watoto ambao hutumia nafasi hii ya kulia kupewa hata vitu vile ambavyo wazazi au walezi hawakupanga kuwanunulia. Kawa mfano kama watapita madukani na mtoto akaikuta baiskeli, mtoto anaweza kuanza kulilia anunuliwe baiskeli ambayo mzazi hakuwa na bajeti hiyo. Mtoto huyo akiendelea kukomaa kulia, mzazi huweza kufanya maamuzi magumu ambayo hakuyapanga.
Mtoto ambaye anakuwa hana tabia ya kulia lia mara nyingine hawezi kusaulika na wazazi na kusababisha kupata mahitaji yake kwa kuchelewa . Kwa mfano kama mtoto atabaikia ametulia kwa muda mrefu bila kulia na mama akawa ‘busy’ na majukumu mengine ni rahisi sana kunyonyeshwa kwa kuchelewa kuliko angekuwa analia. Kama watoto wamezaliwa mapacha vivo hivyo mtoto yule atakayekuwa analia zaidi ndiye atakayekuwa wa kwanza kunyonyeshwa. Hivi ndivyo dunia inavyonyesha watu wake. Utanyonyeshwa pale unapoikumbusha dunia mara kwa mara nini unachokitaka.
Dunia ina kila kitu ndani yake ambapo kila mtu anaweza kuwa tajiri. Naamini swali lililokuja haraka kichwani mwako ni hili, kama dunia ina utele na kila mtu anaweza kuwa tajiri kwa nini matajiri ni wachache kuliko masikini? Jibu ni hili; licha ya dunia kuwa na utele lakini ni bahiri, ni mtu yule tu anayelia sana ndiye anayepokea kutoka kwa dunia. Unahitaji kuwa king’ang’anizi ili uweze kupata kile unachokitaka. Licha ya mipango mizuri unayoweza kuwa umeweka, bado hutaweza kupata kirahisi mpaka pale utakapolia sana.
Watu wengi wameshindwa kupata vitu walivyotaka kwa utele kwa sababu ya kutokuwa waliaji sana. Kuna kiasi kikubwa cha uvumilivu unachotakiwa kukipata ili uweze kupata unachokitaka. Dunia hupima watu kutambua ni kwa kiasi gani umejitoa kupata kile unachokitaka. Ndiyo maana kuna wakati umewaka mipango vizuri ya jambo unalotaka kulikamilisha lakini majibu yanakuja kuwa tofauti na ulivyotegemea. Unahitaji kuendelea kulia.
Anza kulia: Dunia ina utele lakini huwa inawapa wale walioonyesha nia ya kuvipata. Unataka nini maishani mwako. Kitu gani ukikipata au kufanya kitatimiza thamani yako ya hapa duniani? Ni kiasi gani cha fedha ukikipata kitakupa utajiri wa maisha yako? Kuyatambua haya ni mwazo wa kulia. Kutoyatambua haya ni kuamua kunyamaza. Na itakuwa ngumu kunyonyeshwa na utajiri ambao dunia inao. Kuweka bayana nini unakitaka maishani mwako ni mwanzo mzuri wa kuanza kulia.
Endelea kulia: Mara nyingine ulifanikiwa kuanza kulia kwa kuweka mipango yako vizuri. Lakini matokeo yake yameenda tofauti na vile ulivyokuwa umetarajia. Katika hatua hii dunia bado inakuangalia kama kweli una nia ya dhati ya kukipata unachokitafuta. Hata kama mambo ni magumu, mradi tu kama upo kwenye njia sahihi wewe endelea kulia. Kuendelea kutafuata wateja wapya wa biashara yako ni kuamua kuendelea kulia na si muda dunia itakunyonyesha kwa utajiri wake.
Inuka na endelea kulia: Licha ya kuweka jitihada kubwa katika mipango yako lakini mambo hayakukuendea vizuri kisha ukaamua kukata tamaa na kuona dunia haina usawa na haina huruma. Kama upo njia sahihi inakupasa kuinuka tena na kuendelea kulia, ukinyamaza sauti yako haitasikika tena. Jifunze kutoka kwenye anguko kisha endelea kuweka jitihada, dunia itakunyonyesha ukiendelea kulia.
Nini ilichokunyamazisha usiendelee kulia? Ni wakati wako sasa wa kuamuka na kuendelea kulia kwa kuweka jitihada kwenye mipango sahihi ya maisha yako uliyokatia tamaa. Dunia haitavumilia kukuona ukiendelea kulia kwa haki, hivyo usipokata tamaa kwenye mipango yako itakupa unachokitaka. Inuka sasa na endelea kulia. Dunia haiwapendelei walionyamaza.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz