Ni Kitu Kidogo Sana Lakini Kitakupatia Matokeo Makubwa Sana Ukikifanya.
Wote waliofanikiwa na walioshindwa kuna hatua ambazo wanazichukua zinazowawezesha kupata matokeo wanayoyapata. Kwa sababu makundi haya mawili wanapata matokeo tofauti, hii inamaanisha kuwa hata hatua wanazozichukua ni tofauti pia.
Hatua zinazochukuliwa na mtu yoyote hutegemea kitu kimoja kinachoonekana ni kidogo kisichoonekana, lakini chenye nguvu kubwa sana. Inawezekana hakiwekewi uzito mkubwa kwa sababu hakionekani. Kitu hicho ndicho kinachoamua ufanye nini na pia usifanye nini. Hicho ndicho kinachoamua nini ufanye unapokutana na magumu. Hicho ndicho kinachoamua tabia za maisha yako. Kitu hicho ni MATAZAMO.
Mtazamo ni namna ya kuona mambo. Hii ndiyo miwani ya kutazamia dunia. Kama unaiona dunia ni ya rangi ya bluu au njano ni kwa sababu mtazamo wako. Kama unawaona watu ni wabaya wana roho mbaya, ni kwa sababu ya mtazamo wako. Kama unaona matajiri ni watu wabaya na hawastahili kuigwa tambua ni kwa sababu ya mtazamo wako. Mtazamo hauonekani, lakini ndiyo unaoendesha vitendo vyako. Hapo ulipofika ni kwa sababu ya mtazamo wako.
Ulizaliwa ukiwa mtupu yaani ukiwa ‘neutral ‘ juu ya jambo lolote. Lakini kadri ulivyoendelea kukua, watu waliokuzunguka wakapanda mitazamo ndani yako. Kuwa sahihi au sio sahihi, itategemeana na yale uliyoambiwa, kuyasikia na kuyaamini.
Kama ukiangalia maisha yako ukaona huridhiki nayo kutokana na matokeo uliyoyapata, cha kwanza tambua ni kwa sababu ya mtazamo ulio nao. Unaweza kubadilisha eneo la kuishi, unaweza kubadili marafiki, unaweza kuwachukia watu au kuwalalamikia watu, lakini usipobadili hiki kitu kidogo kinachoitwa mtazamo ni kazi bure. Katika eneo lolote unaloona mambo hayaendi sawa, sababu mojawapo kuu ni mtazamo wako. Unahitaji kubadili mtazamo.
Mafanikio ni haki yako. Kuwa na mtazamo huu pekee unakusaidia kuwa na nguvu ya kuyatafuta mafanikio. Mtu ambaye mtazamo wake ni kuona mafanikio ni ya watu fulani si rahisi kuweka mipango juhudi au uvumilivu ili kupata mafaniko hayo. Kila binadamu ana haki ya kuwa na mafanikio na una uwezo huo, jenga mafanikio yako sasa.
Uvumilivu huondoa ukinzani. Kila mipango na jitihada za mafanikio zina ukinzani wake . Si kila unalolipanga litatokea kama unavyotarajia; kuna kushindwa na kukatishwa tamaa pia. Ni wenye mtazamo wa uvumilivu pekee ndiyo wa aoweza kupata chochote wanakitaka kwani watakitafuta mpaka wakipate.
Mafanikio huhitaji muda mrefu. Watu wengi hupenda mafanikio yawe kama kuotesha mchicha au uyoga; yaani upande na kuvuna ndani ya muda mfupi. Mafanikio makubwa na ya kudumu huhitaji kujengwa kwenye misingi yake kwa muda mrefu. Katika kipindi hicho mtu huhitaji uvumilivu kutokana na changamoto atakazokuwa anapitia. Katika mazingira kama haya unahitaji kuwa na mtazamo sahihi kuwa licha ya jitihada utakazokuwa unaweka, utahitaji kuvumilia ili uweze kupata matokeo. Huu ni mtazamo utakakuruhusu uvumilivu.
Furaha sio zao la tukio. Watu wamekosa furaha ya kudumu kwa sababu ya kufikiri inabidi usubiri tukio fulani likufikie au upate kitu fulani maishani ndipo ufurahi. Kumbe kama ukifanikiwa kubadili kufikiri na kuamini kidogo kuwa furaha ni zao la uhai wako hutakuwa na vipindi vya kufurahi. Jenga furaha yako kwenye msingi wa machakato; maisha ni mchakato hivyo jenga furaha yako kwenye mchakato na sio matukio.
Ndugu! Maisha yako yanaweza kubadilika tu, kwa kubadili mtazamo wako. Ni kitu kidogo, lakini kitabadili kabisa vitendo utakavyokuwa unachukua na kisha kupata matokeo tofauti. Ni maeneo gani umekwama maishani mwako, je kwenye fedha, mahusiano, afya? Anza kwa kubadili mtazamo na kuwa na mtazamo sahihi kisha fanya kwa usahihi.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz