Hivi Ndivyo Umekuwa Ukizima Moto Kwa Petroli.


Categories :



Petroli si inawaka! Itatumikaje tena kuzima moto? Inawezekana huu ni mshangao na swali ulilojiuliza baada tu ya kusoma kichwa cha makala hii. Lakini inawezekana wewe ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakifanya hivyo. Endelea kusoma ujue ni kwa namna gani umekuwa ukizima moto kwa petroli.

Petroli ni miongoni mwa mafuta yanayotumia kufua nguvu kwenye mitambo mbalimbali kama magari na jenereta. Moja ya sifa ya mafuta, haya ni kushika moto kirahisi na hivyo kulazimika kuwa na vizimia moto pale mafuta haya yanapouzwa au kuuzwa. Kwa sababu ya sifa hii ya kushika moto kirahisi hakifai kuwa kimiminika kimojawapo cha kuzimia moto. Hivyo mtu akikukuta uhifadhi petroli ndani au unatembea nayo kwa lengo la kuzimia moto atakushangaa kwani kujaribu kuzima moto kwa petroli ni kuuchochea mara dufu.


Lakini hivi ndivyo umekuwa ukifanya au ukijaribu kufanya katika maisha yako. Kuna matendo ambayo huwa unayatenda ambayo yanazidi kuharibu hali mbaya na kuzidi. Au kwa kuacha kufanya ndivyo unavyozidi kuharibu zaidi hali hali kuwa mbaya zaidi.

Kuridhika na hali mbali uliyonayo ni kuzima moto kwa petroli. Hakuna kinachoweza kubadilika kama wewe hutachukua hatua ya kubadilika. Kama hufanyi chochote kubadili hali uliyonayo, itazidi kuwa mbaya. Usiridhike jinsi ulivyo, hali yako itakuwa mbaya zaidi.

Kulalamikia watu wengine kwa maisha yako ni kuzima moto kwa petroli. Kama una tatizo na unalalamika unakuwa unaziba njia ya kupata utatuzi. Hii ni kwa sababu hakuna ukomo wa kulaumu. Unavyoendelea kulaumu ndivyo unavyoendelea kuchochea hali inayokuandama kuwa mbaya zaidi kwa sababu kutokuwa na uwezo wa kuchukua hatua.

Kujenga tabia ya kuahirisha ni kuzima moto kwa petroli. Kama unataka matokeo lazima uwe na nidhamu kubwa ya kuchukua hatua pale inapotakiwa. Kuahirisha ni kulaza matokeo na hali kuwa mbaya zaidi. Watu wengi wameendelea kuishi maisha ya shida kila siku kwa sababu ya kuahirisha. Kuanzia sasa acha kuahirisha mambo ili usizime moto kwa petroli.

Kulipa kisasi ni kuzima moto kwa petroli. Nini huwa unakifanya pale unapokosewa na mtu mwingine? Nini huwa unakifanya pale unapoonewa? Je unawasamehe? Au unalipa kisasi? Kulipa kisasi ni kuharibu zaidi kuliko kusamehe. Kulipa kisasi ni kutengeneza huzuni zaidi. Kulipa kisasi ni kuweka moto kwenye petroli.

Kuukumbatia uvivu wakati maisha yako ni magumu. Kitu kimojawapo unachotakiwa kukitupa ili uweze kupiga hatua ni uvivu. Miili yetu ina uvivu kwa asili. Ili uweze kupiga hatua huna budi kuuvua uvivu wako. Hii huja kwa kujilazimisha kufanya vitu hata pale unapojisikia umechoka. Kuacha kufanya kazi kwa sababu hujisikii ni kupalilia kushindwa hii ni sawa na kuzima kushindwa kwa kutumia petroli.

Chunguza maeneo mbalimbali ya maisha yako. Ni wapo unajaribu kuzima moto kwa petroli? Ni tabia gani unaona unatakiwa uziache lakini bado unazifanya na hivyo kuendelea kuchochea kushindwa? Usizime moto kwa petroli.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *