Hivi Ndivyo Unavyoweza Kufua Umeme Maishani Mwako.


Categories :



Maji yakiachwa na kutawanyika huonekana hayana nguvu na kila mtu huyadharau. Pia nguvu yake huwa ndogo. Lakini kiasi hicho hicho cha maji kikikusanywa na kuelekezwa kupita kwenye bomba, mgandamizo wake huongezeka na kuwa na uwezo hata wa kufua umeme.

Hivi ndivyo inavyoonekana kwa watu wengi hapa duniani. Wengi wameoneakana ni watu wa kawaida kwa sababu ya kuhangaika na vitu vingi kwa wakati mmoja. Kwa kufanya hivyo wametawanya nguvu na kuonekana hawana madhara yoyote katika maisha yako. Wamefanya hivyo kwa kuendelea kugusa hiki na kuacha kisha kushika kitu kingine. Naamini umeshawashuhudia mtu akianzisha kila biashara inayokuja. Hata kama alikuwa na biashara anayoiendesha, akisikia kuna biashara mpya inalipa zaidi huiacha biashara hiyo.

Umehangaika na kuzunguka kwa muda mrefu  kwa ajili ya maisha yako lakini unahisi bado hujafanya kitu chochote cha maana. Unaona hata ukifa leo utasahaulika haraka kwa sababu watu watakosa cha kukukumbuka kwacho. Hii ni kwa sababu hakuna kitu kimoja ulichochagua na kuamua kukomaa mpaka kufanikiwa kupata matokeo makubwa yaliyoishangaza dunia.


Ni kweli licha kuishi kwa muda mrefu na kufanya vingi lakini havionekani kwa sababu ya kugusa vitu vingi. Yaani ulianza kitu, kabla hujakikuza na kufikia ukubwa wake ulikiacha na kuhamia kufanya kitu kingine.  Pia hukutaka kufanya jambo moja au machache kwa wakati ukifikiri ndiyo ungeweza kufanya makubwa. Mwisho wa yote umeambulia kidogo kidogo kwenye baadhi ya vitu ulivyokuwa unafanya. Kila mtu ana uwezo wa kufanya kwa kugusagusa na kupata matokeo madogo ambayo hayawezi kukushangaza na kukuridhisha hata wewe mwenyewe.

Matokeo unayoyapata kwa kugusagusa bila kuzama ba kufanya kwa ukuu ni ya kawaida na yamekufanya kuwa mtu wa kawaida pia. Licha ya kila mwanadamu kuumbwa na upekee, upekee huo hupotelea kwa kuendelea kufanya vitu kwa kugusagusa. Uwezo wako wa pekee ulikuwa kwa ajili ya kukusaidia kufanya vitu kwa upekee na kwa kubobea.

Kuna jambo moja muhimu la kufanya sasa baada ya kuambulia kidogo licha ya kufanya mambo mengi. Jambo hilo ni kukusanya, ndiyo kukusanya nguvu na kuelekeza kwenye jambo moja ua machache. Badala ya kutawanya nguvu na muda wako kwenye mambo mengi sasa nguvu na muda wako ekeleza kwenye mambo machache. Komaa na jambo hilo mpaka kufikia ubobezi na mafanikio makubwa.

Kubobea kunakuja baada ya kutambua vitu unavyovipenda kuvifanya na unaweza kuvifanya vizuri. Baada ya kutambua eneo lako la kipekee ndipo unapoanza kuwekeza nguvu kubwa kuhakikisha unafanya kitu hicho kwa ubora wa hali ya kiasi cha mtu mwingine kutokukufikia kirahisi. Naamini utakuwa umeshuhudia mtu mmoja anayeamua kuchagua hata kufanya biashara fulani kiasi cha mtu akifikiria kuhusu biadhaa fulani wazo la kwanza linakuwa kuhusu bidhaa za mtu huyo kwanza.

Ubobezi upo kwenye kila eneo kwa mfano kwenye sanaa na uongozi pia. Kwenye eneo lolote unalolipenda na kuona unaweza kufanya vizuri una nafasi ya kuamua kuchimba kwa ndani na kutoa thamani kubwa sana kwa watu wengine.

Acha kuhangaika na mambo mengi sasa na kutawanya nguvu zako. Ni muda wa kuanza kukusanya nguvu zako baada ya kuhangaika kwa muda mrefu. Kufanya hivyo  ni sawa na kuyakusanya maji na kuyaelekeza kwenye bomba jembamba,  ambapo sasa huwa nguvu kibwa kiasi cha kufua umeme. Usifanye mambo mengi tena kwani kufanya hivyo unapoteza nguvu na muda mwingi, kwani kila unapoanza jambo jipya unatumia muda na nguvu nyingi. Bali ukijikita na jambo moja nguvu na muda wako utatumika kukuza kitu ambacho tayari unacho.

 Chukua hatua: Tafakari mambo mengi uliliyokuwa unafanya, kisha chagua jambo moja ambalo utawekeza nguvu na muda wako wote kuhakikisha unapata mafanikio makubwa. Kusanya nguvu zako sasa na kuzielekeza kwenye bomba moja. Kwa kufanya hivyo utaweza kupata nguvu kwa pamoja zitakazoweza kuzungusha mipango yako mizuri uliyoweka na kuzalisha umeme wa mafanikio.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz
 




Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *