Kwani Unasubiri Nini?
Nitafanya kesho. Nikipata kitu fulani nitafurahi sana! Mambo yangu yakiwa mazuri nitaanza! Ningekuwa kama fulani nimefanikiwa! Serikali ingekuwa inafanya hiki mambo yangu yangenyooka! Wazazi wangu wangenisomesha nisingekuwa hivi.
Hizi ni kauli zilizozoeleka miongoni mwa watu. Hizi kauli zinazoonesha kuna kitu mtu anahisi amepungukiwa hivyo kumfanya aendelee kusubiria au kuwa na sababu ya msingi ya kutofanya au kupata kitu fulani. Hizi ni kauli ambazo mtu huzitoa ili kuhalalisha hali aliyo nayo na kutokuwa na jitihada zozote kujikwamua.
Ndugu mtu wa kwanza wa kuchukua jukumu la maisha yako ni wewe. Mtu pekee ambaye ataamua uwe na maisha ya namna gani ni wewe. Mtu pekee wa kuhakikisha unafanikiwa au unashindwa ni wewe. Mtu pekee wa kuwa na uchungu na maisha yako ni wewe. Mtu pekee ya kubadili maisha yako kutoka kwenye hali uliyonayo sasa na kuwa bora zaidi ni wewe. Unasubiri nini kuanza kuchukua jukumu lako?
Umeendelea kukumbatia hali mbaya ya maisha uliyonayo kwa sababu ya kuona kama unahitaji kumsubiri mtu au kitu fulani hivi kuja kubadili maisha yako. Nikuhakikishie kuwa utasubiri sana na hakuna kitakachobadilika. Kuna siku pekee ambayo hali maisha yako yataanza kubadilika, ni siku ile utakayotambua na kukubali kuwa hakuna kitu cha kuendelea kusubiri ili kuboresha maisha yako bali kuchukua jukumu la maisha yako.
Unasubiri nini kuwa tajiri? Kila mtu anatamani kuwa tajiri. Kila mtu anatamani angekuwa na utele kwenye kila eneo la maisha yake. Japo utajiri wa fedha au mali ndiyo unaopewa kipaumbele na watu wengi. Lakini licha ya kuwa na tamaa hii, kumekuwa na kasumba ya kuona kuna watu fulani au kitu fulani ambacho inabidi ukisubiri ili upate huo utajiri. Mara nyingine umeona serikali ndiyo yenye jukumu la kukupa utajiri huo. Msingi wa utajiri ni thamani, wape watu thamani kubwa nao watakupa utajiri.
Unasubiri nini kuwa na furaha? Je mpaka uwe tajiri ndiyo uwe na furaha? Je utakuwa na furaha baada ya kufanikiwa kwenye jambo fulani. Furaha yako itakuwa ya kudumu kama utafanikiwa kuijenga kwenye mchakato wa mambo unayoyafanya badala ya kuweka kwenye matukio. Unasubiri nini kuwa na maisha ya furaha wakati wote?
Unasubiri nini kuanzisha biashara? Ni muda mrefu sana umekuwa ukijipanga kuanzisha biashara! Kila ukifikiri kuanzisha biashara unasema bado sijajipanga na sasa muda umeenda sana. Unasubiri nini? Nakushauri uianze biashara yako sasa haya kwa chochote ulichonacho. Hakuna siku utakayoona umekamilika kwa kila kitu. Anza na chochote ulichonacho kisha endelea kuboresha kila siku.
Vitu ulivyovitamani kwa muda mrefu sana unaweza kuvipata kwa kuamua kuchukua jukumu hilo la kuvipata kwa asilimia mia moja. Usiendelee kusubiri chochote au yoyote, anza mwenyewe kwani hakuna mwingine wa kukuwezesha. Vitu gani umevisubiri kwa siku nyingi ukiamini vitakuja? Chukua jukumu hilo la kufanya mwenyewe.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz