Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukimbia Hata Kama Huioni Miguu Yako.
“Licha ya jongoo kuwa na miguu mingi lakini hushindwa kasi na nyoka ambaye hana hata mguu mmoja”
Kama uwingi wa miguu ungekuwa ndiyo kigezo pekee cha kasi ya kutembea, basi jongoo angekuwa na kasi hata ya kuzidi kasi ile ya farasi. Lakini licha ya jongoo kuwa na miguu mingi bado ana kasi ndogo hata kuliko nyoka ambaye hana hata mguu mmoja unaoonekana.
Kuna wakati umeona unahitaji kuwa na vipaji vingi ili uweze kufanikiwa. Hata kile kimoja ulichonacho hujakitumia vilivyo kwa kuamini kuwa mafanikio utayapata kwa kuwa na vipaji vingi. Ukiwaangalia waliofanikiwa unadhani kuwa wao wana vipaji vingi walivyonavyo vinavyofanya wao wafanikiwe zaidi ya wewe. Ukijiangalia wewe hatua ulizopiga unajiona kuna vitu umepungukiwa. Kama ni vipaji unajiona wewe huna au unavyo vilivyo dhaifu.
Kadhalika umeamini kuwa ili uweze kufanikiwa unahitaji mtaji mkubwa ili uweze kuwa na lengo la kuwa na biashara. Ukiangalia biashara kubwa zinazokuzunguka, unadhani kuwa wenye biashara hizi walipata bahati ya kupata mitaji mikubwa mara moja na kuanzisha biashara hizi zilizokua na kudumu mpaka leo. Ulivyoangalia na kuona hakuna mtaji unaokuzunguka ukaamini kuwa huwezi kuanzisha na kuendeleza biashara yako. Hiyo ni dhana potofu, hata hao unaowaona wapo kileleni hawakuanzia hapo, na wala hawana kitu ambacho wewe huna, au vipaji vingi kuliko wewe. Hivyo na wewe una nafasi ya kufanya vikubwa kama wao kama utatambua nini kilichopo ndani yako na kukitumia kwa uaminifu bila kujali huo udogo unaoupa.
Umekuja duniani ukiwa umekamilika. Una kila kitu ndani yako cha kukufanya upate mafanikio yoyote unayoyataka. Hata kama huoni una uwezo au vipaji vinavyokuwezesha, lakini nakuhakikishia kuwa umekamilika. Wewe ni zaidi ya gari lile linaloachiwa kiwandani ili liuzwe kwa ajili ya matumizi. Mpaka linatolewa kiwandani linakuwa limeshajaribiwa na kuona linaweza kufanya kazi ile ambayo limekusudiwa. Hivyo hupo hapa duniani ukiwa hujakamilika. Kazi yako ni kutambua ukamili wako na kuutumia kufanya mambo makubwa.
Kitu cha kwanza cha kwanza unachotakiwa kuanza nacho ni kujiamini mwenyewe kuwa lazima una kitu ndani yako hata kama hukioni cha kukuwezesha kupiga hatua kubwa. Kisha uliza moyo wako na akili yako nini inahitaji kupata katika maisha yako. Kile ambacho moyo wako utakitaka kwa hali yoyote ndicho kilichobeba upekee wako.
Anza kuweka kazi kwa kutumia hichohicho unachofikiri na kisha. Kadri unavyoendelea kuweka malengo ambayo yatahitaji nguvu zaidi ya zile ulizozizoea, ndipo utakapoanza kuona uwezo uliopo ndani yako ambao hujawahi kudhani unao. Kitu gani moyo wako umekuwa ukikukumbusha kukifanya licha ya wewe kukipuuzia. Huu ndiyo wakati wa kuanza kuuitikia moyo wako ili uanze kutembea kwa kasi kubwa hata kama unadhani huna majibu.
Usiache kuishi maisha yako kikamilifu kwa kufikiri huna uwezo wa kukamilisha. Uwezo huo unao hata kama unaona ni kidogo. Kinaonekana kidogo kwa sababu hujakipa mzigo mkubwa wa kubeba. Anza kwa kujipa lengo dogo na baada ya kulikamilisha jipe kubwa zaidi. Ndipo utakaposhangaa nguvu ambazo umekuwa nazo kwa siku nyingi lakini ulikuwa huzitumii.
Chagua leo nini unakitaka maishani mwako kisha weka mipango huku ukiamini una nguvu za kutosha. Usijiwekee mipaka katika kuchagua, bali amini una kila kinachoweza kukufanikisha.
Chukua hatua: Chunguza mambo yako uliyosita kuchukua hatua kwa kuamini huna uwezo wa kuyakamilisha. Yawekee malengo na mipango wa kuyatimiza kwa una uwezo huo ndani yako. Anza hata kwa hatua ndogo, kisha weka malengo makubwa zaidi kila mara ili kujisukuma kuamusha uwezo mkubwa uliolala tu ndani yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz