Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutumia Sumaku Iliyopo Ndani Yako Kuvuta Mafanikio.
Ukichukua unga wa chuma na kuusogeza karibu na sumaku, unga huo utavutwa kwenye sumaku. Sumaku haitakuwa na mjadala kama ivute chuma hicho au la. Lakini ukichukua unga wa mahindi na kuweka karibu na sumaku hakuna kitakachoendelea zaidi ya kubaki vinatazamana.
Nguvu ya sumaku kuvuta chuma ipo ndani yako ambayo unaweza kuitumia kuvuta mafanikio katika maisha yako. Unaweza ukaanza kutafuta ni wapi sumaku yako ipo! Lakini una sumaku ndani yako ambayo ina uwezo wa kuvuta mafanikio ndani yako japo watu wengi wamekuwa hawaitumii. Sumaku hiyo ni akili yako. Ili upate chochote maishani mwako, ni lazima kivutwe na kukaa kwanza kwenye akili yako ndipo baadaye kiweze kuonekana katika mazingira ya nje.
Akili kama sumaku huvuta mawazo kwa njia ya kusikia, kuona, kufikiri, kunusa nk. Kisha mawazo hayo yakijengeka ndani yako yanavuta vitendo utakavyokuwa unafanya na matokeo utakayopata. Kumbe nini unakipanga kukufanya ua unachokijibu baada ya kukutana na changamoto kinategemeana na mawazo yaliyovutwa na akili yako na kukaa humo.
Bahati mbaya akili ni sumaku yenye uwezo wa kuvuta mawazo hasi pia. Haya ni mawazo ambayo yakivutwa akilini mwako huzaa vitendo ambavyo vinaweza kukuharibu maisha yako. Una uchaguzi wa nini akili yako ivute. Weka chujio kwenye akili yako ili iweze kupitisha mawazo chanya yatakayokupa mafanikio. Hivi ndivyo unavyoweza kutumia sumaku ndani yako kuvuta mafanikio;
Fikiri chanya muda wote. Unavuna unachopanda. Ukipanda mahindi shambani usitarajie kuvuna mpunga. Kwa sababu akili itazalisha chochote kitakachovutwa na kukaa kichwani mwako kwa muda mrefu, basi wewe chagua kufikiri mawazo chanya kila wakati ili uvune mafanikio. Epuka kukaa na watu wanaoongea hasi kila wakati, wanaolalamika kila wakati, wanaowasema watu wengine kuongea habari nyingine zinazofanana na hizo.
Fikiri kwenye utele. Huwezi kuweka juhudi ya kupata utajiri kama akili yako inaamini kuna uhaba. Dunia kwa asili ina utele, inakuhitaji wewe tu ujipange ili uweze kuvuna utajiri uliopo. Ona na wewe ni tajiri, fikiri na tenda kitajiri. Ukifikiri kitajiri utavuta matendo ya kitajiri, watu matajiri, mbinu za kitajiri nk.
Fikiri uimara. Una udhaifu na uimara ndani yako. Ili uweze kupata matokeo yatakayokupelekea mafanikio huna budi akili yako kufikiri uimara ulionao na jinsi unavyoweza kuutumia kwa ufanisi mkubwa. Kuwekeza nguvu kwenye kufikiri udhaifu usioweza kuubadili, ni kuamua kupoteza muda na umakini. Uimara ulionao ndiyo ulioumbiwa kutenda miujiza, ufikiri huo vyema na utakuzalia mafanikio.
Fikiri upendo. Unaweza kutoa thamani kwa watu wengine kwa sababu ya upendo. Maisha yako yatakuwa ya furaha kama utakuwa unafikiri upendo muda wote na si chukua. Unavuna unachopanda. Ukipanda chuki, visasi na malalamiko ndiyo utakayovuna, bali ukipanda upendo, amani, msamaha na mengine yanayofanana na hayo ndiyo utakayovuna.
Ndugu! Una sumaku ndani yako ambayo inaweza kuvuta chochote katika maisha yako. Hii ni nguvu kubwa ya akili yako inayoweza kukupa chochote unachota. Uthibiti wa nini ukifikiri upo mikononi mwako. Unataka kuwa mtu namna gani maishani mwako? Unataka utajiri maishani mwako? Unataka amani na upendo maishani mwako? Unaweza kuvipata kwa kuviwaza hivyo muda wote.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz