Iga Kitu Hiki Wanachokifanya Waliofanikiwa Baada Ya Kushindwa.
“Ili mcheza mieleka ashinde, hutamani mshindani wake asiamuke baada ya kuanguka chini. Kuamka kwa mshindani wake huona mashindano yakianza upya”
Hakuna ambaye hajawahi kujikwaa na kudondoka katika kutembea kwake. Kujikwaa na kudondoka si habari inayoshtua, habari inakuwa pale unapoanguka na kuendelea kulala palepale. Mtu ukianguka watu hutarajia kuwa utaamuka kisha kujiangalia madhara ambayo umeyapata kwa kuanguka huko. Baada ya hapo ulianguka hutarajiwa kuwa utaendelea na safari yako kama kawaida. Lakini hushituka na kushangaa pale wanapokuona huamki na unaendelea kulala palepale ulipoanguka.
Kuna kushindwa katika maisha, hata ukiwauliza walifanikiwa sana katika maisha yao, kuna wakati walishindwa. Kuna wakati walianguka katika wakiendelea kupiga hatua za kufikia mafanikio yao. Kuna wakati walipata upinzani mkubwa kwenye biashara zao zikafa, lakini wakarudi tena. Kuna wakati waliibiwa na kupoteza kila kitu, lakini wakajipanga na kukusanya mtaji na kuendelea na biashara zao.
Lakini kilichowafanya kufanikiwa katika safari ya maisha yao ya mafanikio ni kutokubali kushindwa. Walipoanguka hawakukubali kuendelea kulala hapo, bali waliinuka, wakajikung’uta mavumbi kisha wakaendelea na safari.
Watu wengi wanachokiona kwa mtu aliyefanikiwa ni mafanikio aliyonayo kwa muda huo na sio njia alizopita na kwa namna gani. Kuna historia za kutisha za kushindwa ambazo ungepata nafasi ya kusimuliwa, ungejishangaa ni kwa nini wewe uliamua kukata tamaa haraka hivyo.
Mgunduzi wa taa za umeme, Thomas Edison alipitia safari ndefu sana mpaka kufikia mafanikio mkubwa ambayo yanaimbwa leo na yataendelea kukumbukwa katika historia ya dunia. Walimu wake walisema alikuwa mjinga sana wa kujifunza chochote. Kabla ya kuanza majaribio ya uvumbuzi wa taa hizo alikuwa tayari ameshafukuzwa kwenye kazi mbili.
Kama mvumbuzi, alifanya majaribio elfu moja mpaka kuja kufanikiwa kugundua balbu ya umeme. Haya ni majaribio mengi sana ukijaribu kulinganisha na uliyofanya wewe. Mara ngapi umefanya kitu mara moja tu na baada ya kushindwa ukaacha na kwenda kufanya kitu kingine. Mara ngapi umeanzisha kitu, baada ya kufanya kidogo tu ukasema hiki kitu ni kigumu sana ukaamua kukiacha na kwenda kutafuta cha rahisi ambacho hakina thamani?
Tatizo kubwa ambalo linawakumba watu wengi na kushindwa kupiga hatua kubwa ni mtazamo wanaokuwa nao juu ya matokeo wanayoyapata baada ya kuweka jitihada zao. Je huwa unafikiri nini ukipata matokeo ambayo hukutarajia? Edison aliulizwa na mwandishi wa habari kuwa alijisikiaje baada ya kufeli mara elfu moja? Edison alimjibu mwandishi kuwa hakushindwa mara elfu moja bali ugunduzi wa balbu ulichukua hatua elfu moja.
Hili ni jibu linaloweza kubadili mtazamo wako juu ya kushindwa. Unapochukua hatua na kushindwa, kumbuka huko sio kushindwa, bali umechukua hatua mojawapo ya kusogea kwenye mafanikio yako. Wengi huona kushindwa ni kosa, si hivyo, bali ni hatua za kusogelea ushindi wako.
Unaposhindwa, jiambie kuwa nimepiga hatua mojawapo kuelekea kwenye mafanikio. Lakini ili ufikie mafanikio hayo haraka inakupasa ujifunze kutokana na kushindwa huko ili wakati mwingine usianguke palepale. Kama ikitokea unaanguka basi iwe mbele zaidi na ulipoanguka mara ya kwanza na pia iwe karibu zaidi na kilele.
Je kuna vitu gani vimekuangusha katika kutimiza malengo ya safari yako ya mafanikio? Je mtaji, ushindani, maarifa, mahusiano au afya? Usikubali kukata tamaa, amka jifunze ili usianguke tena eneo hilo kisha endelea na safari japo kiugumu, ukiendelea kupiga hatua hata kama ndogo utafanikiwa tu.
Chukua hatua. Baada ya kuanguka, inuka jifunze kisha endelea na safari yako ya mafanikio. Neno kushindwa lisiwe miongoni mwa misamiati ya kamusi ya maisha yako. Wapi ulianguka unatamani uinuke leo?
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz