Dunia Imekuhadaa


Categories :

Ulipokuwa mtoto ulikuwa mtulivu ukifanya uliyoyafikiri wewe, yaani ya ndani mwako. Ulikuwa unacheka sana bila ya kujali nani alikuwa anakuona. Chochote ulichotaka ulijaribu kukipata hata kile kilichoonekana kuwa mbali na wewe, ukiamini unaweza kukifikia. Uliamini hakuna kinachoshindikana, ulijaribu kufanya vitu vingi ukiamini utafanikiwa. Haya yote yaliwezakana kwa sababu uliyasikiliza toka ndani mwako, hayakuwa maoni ya watu wengine.

Kadri ulivyoendelea kukua ulianza kupata maoni ya watu kuhusu yale uliyokuwa unayasikiliza na kuamini toka moyoni mwako. Ulisikiliza maoni ya wazazi au walezi, walimu na jamii pia. Wazazi walijaribu kukulinganisha na watoto wengine, ndugu zako au jirani na kukuambia labda wewe hupovizuri kwenye jambo fulani kama hao. Walimu walikufanyisha mitihani na ulipofeli wakakuambia huna akili.

Dunia ilianza kukuaminisha kwa nini baadhi ya vitu ulivyo kuwa unavihitaji haviwezekani.Kadri ulivyoendelea kukua umesikiliza mambo mengi na ndiyo yaliyojaa ndani mwako. Hizi zimekuwa ni kelele nyingi za dunia ambazo zimepoteza uhalisia wako. Husikilizi tena sauti ya moyo wako, ya wewe ni nani? Nini upekee wako? Kelele hizi zimekufanya uione dunia ya uongo. Unavyoiona dunia kwa sasa ni kwa mujibu wa mtazamo wako ambao umetokana na maoni au kelele za dunia ulizozisikiliza kwa muda mrefu. Maoni ya dunia yaliyojazwa kwenye fikra zako yamekuvalisha miwani ambayo yanakufanya uione dunia kupitia maoni hayo na sio uhalisia.

Hivyo na wewe mwenyewe umepoteza uhalisia wako badala yake umekuwa ‘’fake’’.

Umeshindwa kusikiliza sauti ya ukuu kutoka ndani ya moyo wako kwa sababu kila wakati umekaa kwenye kelele nyingi za jamii. Kelele hizo zimekufanya kuishi maisha ya kuiga na sio kulingana na kusudi na uwezo wako halisi. Maisha ya kuiga yamefifisha uwezo wako mkubwa ulio ndani yako. Umekuwa ukiishi chini ya kiwango, ukitumia uwezo wako kwa kiwango kidogo sana kwa ajili ya kuiga kundi badala ya kuwa wewe na kuishi upekee.

 Nina habari njema kuwa una uwezo wa kuachana na “ufake” ulioutengeza na kurudia uhalisia wako.

Njia mojawapo ya wewe kurejesha uhalisia wako ni kutoka nje ya kundi la jamii ambako kuna kelele nyingi, kujitenga na kuanza kusikiliza nafsi yako.  Hii itakusaidia wewe kujiuliza maswali kama wewe ni nani? kwa nini upo hapa duniani? na nini upekee wako? nk.  Kupata majibu ya maswali kama haya itakusaidia kujua uhalisia wako.

Mafanikio makubwa nay a kweli utayapata ukifanikiwa kutoka kwenye wewe fake na kuwa wewe halisi. Ukiwa na kuishi uhalisia wako utafanikiwa kuamsha uwezo wako mkubwa ulio lala ndani yako na kufanya makubwa. Kwa kuwa wewe halisi utafanikiwa kuishikusudi lako na kupata mafanikio yenye ridhiko la moyo.

Kaa chini leo na jiulize kama wewe ni fake au ni halisi? Kama chini na uusikilize moyo wako nao utakuambia ukweli kuhusu wewe kasha chukua hatua halisi kupata mafanikio makubwa unayostahili.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa Uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.ac.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *