Kasi Kubwa Ya Kinyonga Hujulikana Pale Msitu Wake Unapochomwa Moto.
Kinyonga ni kiumbe aliyopo duniani anayesemwa kuwa na mwendo wa pole pole na wa maringo. Ukimuona anatembea kutoka jani moja kwenda jingine, utadhani kuwa hana safari kwani muda mrefu utapita, lakini utaona kama amebakia palepale .
Lakini habari huwa tofauti pale ajali inapotokea na hasa moto. Kama hujawahi kushuhudia upande mwingine, ndipo unapoweza kuona upande mwingine wa kiumbe huyu mwenye sifa ya kutembea polepole. Waswahili wanasema ukitaka kujua mbio za kinyonga choma msitu. Kukiwa na moto unawaka karibu na kinyonga, ndipo huonyesha kasi yake aliyonayo na wewe mtazamaji ukarekebisha mtazamo uliokuwa nao. Katika mazingira kama haya, kinyonga huacha maringo yake na kukimbia kwa kasi kubwa ili kujiokoa.
Changamoto kimekuwa kichocheo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Ili aweze kufikiri kwa utofauti, ili aweze kubadili tabia, ili aweze kufanya tofauti na mazoea, binadamu anahitaji jambo la kufanya hivyo hata kwa kulazimishwa. Mazingira hayo humsaidia kuamsha uwezo wake alionao ndani yake ambao ukiwa umelala tu. Na ni katika mazingira ya changamoto ndipo unapoweza kumuona mtu akifanya kwa kiwango cha juu tofauti na mazoea. Yafuatayo ni mazingira ambayo changamoto humsaidia mtu kufanya kwa ukubwa zaidi na mazoea.
Mtu anapokimbizwa na simba ndipo utajua kuwa ana kasi zaidi. Anaweza kuwa mtu unayemfahamu, mwenye mwendo wa goigoi lakini ikitokea akamuona simba na kutambua ni mbio tu zitaokoa uhai wake ndipo utabahatika kuiona kasi ambayo hujawahi kuiona kwake. Hii ni kasi amabaye usingeweza kushuhudia kama asingekimbizwa na simba.
Mtu anapozama majini ndipo anapojaribu kuogelea. Ukipata ajali ya maji na hivyo ukawa kwenye hali ya kuzama, ndipo unapoweza kufikiria na kujaribu kuogelea kitu ambacho hukuwahi kukifikiria hapo awali. Hii inakuwa nafasi ya kuamsha nguvu ambayo bila ajali hiyo usingeweza kuamsha uwezo huo. Hivi ndivyo changamoto zinavyoweza kukuwezesha kufanya nje ya mazoea.
Mtu anapokosa fedha ndipo anakuwa tayari kufanya kazi yoyote. Kama una fedha ya kukidhi mahitaji yako muhimu, unaweza usiwe tayari kufanya kazi yoyote ile ile kukuingizia kipato. Katika kipindi hicho, utakuwa mchaguzi sana, bila kujali kuwa unahitaji kukufanya zaidi ya unavyofanya muda huo ili kufikia utajiri. Lakini hali hubadilika pale unapokuwa kwenye uhaba wa fedha hata ile ya kupata mahitaji muhimu ya maisha kama vile chakula. Katika hatua hii ndipo mtu anakuwa yupo tayari kufanya kazi yoyote ile mradi tu itampa kipato cha kufanya aendelee kuishi. Hili ni somo kuwa kila wakati tafuta changamoto ambayo itakufanya utoke nje ya mazoea. Kuwa na ndoto kubwa unayoiishi kwa muda huo.
Ndugu! Huwezi kufanya mambo makubwa bila kujipa changamoto zitakazokutoa kwenye mazoea. Tayari una maisha fulani uliyoyazoea. Huwezi kupata matokeo mapya kama hutapata msukumo wowote kutoka nje. Kama una malengo ambayo umekuwa ukiyafanyia kazi na kupata majibu, huwezi kukua zaidi ya hapo bila kujipa changamoto mpya. Changamoto mpya itakuwa ni kujipa malengo makubwa kuliko uliyonayo sasa.
Chukua Hatua: Tafakari eneo la maisha ambalo unataka kuliimarisha; fedha, afya, mahusiano, kazi, au biashara kisha jipe jukumu kubwa zaidi ya yale uliyoyazoea kufanya na kukamilisha. Ukifanikiwa kukamilisha hilo, jipe tena lengo kubwa zaidi ya ulilokamilisha. Hii itaamusha uwezo wako wa ndani na kukusaidia kufikia mafanikio makubwa.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz