Usijipunje! Unajilinganisha Na Nani?


Categories :

Tupo zaidi ya watu milioni 8 duniani  kwa sasa. Ni idadi kubwa sana ya watu na unaweza kufikiri kuwa kuna nafasi wewe kufanana na mtu mwingine.  Lakini nikuhakikishie rafiki yangu kuwa hakuna mtu yoyote unayefanana na wewe kwa kila kitu. Hii inamaanisha kuwa licha ya kufanana na mtu mwingine, lakini bado kuna utofauti ulionao ukilinganisha na watu wengine.

Kila aliyeumbwa hapa duniani ana kusudi maalumu la kulitekeleza. Sungura ni majanga sana lakini ukimweka kwenye maji, ujanja wake unaisha, hataweza kuogelea. Kadhalika zoezi la kuogelea kwa samaki ni jambo rahisi sana akiwa majini.

Hivyo na wewe una upekee mkubwa ndani yako. Kutokana na upekee ulionao, hukutakiwa kufanya vitu kwa kujilinganisha na watu wengine. Jambo hili ni sawa na wanafunzi wawili waliokaa chumba kimoja lakini wanafanya mitihani miwili tofauti.  Hivyo wakiangaliana watakuwa wanajidanganya.

Kujilinganisha na mtu mwingine ni kujiaminisha kuwa wewe unafanana na watu wengine kwa kila kitu; yaani wanachokifanya wengine na wewe ndicho kinachokufaa. Kwa kufanya hivyo unafuta upekee ulionao ndani yako. Hili ni kosa ambalo watu wamekuwa wakilifanya. kila binadamu yupo hapa duniani kwa kusudi maalumu ambalo halifanani na mtu mwingine. Kwa kuwa na kusudi maalumu umewekewa uwezo wa kipekee ili uweze kutimiza kusudi hilo kikamilifu. Hivyo si halali kulinganisha uwezo wako na wa mtu mwingine kwani kila mtu ana kazi maalumu ya kuikamilisha.

 Njia sahihi ya kulinganisha uwezo wako ni kuoanisha kiasi ulichotumia na kile ulichonacho. Ukifanya hivyo ndipo utajua ni kwa kiasi gani bado una uwezo mkubwa ndani yako ambao bado haujatumika. Kujilinganisha na mtu mwingine ni kujipunja kwani wengi hujilinganisha na watu waliopata mafanikio baada ya kutumia kiasi kidogo tu cha uwezo wao. Kwa sababu ya kusudi tofauti, kujilinganisha na mwingine kunaweza kukakukatisha tama baada ya kuona wewe huwezi kuyapata mafanikio hayo ingali wewe una mafanikio tofauti na hayo.

Zifuatazo ni hasara za wewe kujilinganisha kiuwezo na mtu mwingine;

Kujilinganisha kumesababisha watu kuishi nje ya kusudi. Kama utakuwa anaangalia fulani anafanya nini ili na wewe ufanye basi huishi maisha yako. Kama huishi maisha (kusudi) yako basi unasaidia kuishi maisha ya mtu mwingine kwa kujilinganisha naye.

Kujilinganisha kumesababisha ujipunje uwezo wako. Ukiwianisha mafanikio uliyoyapata na kile wengine wamepata, kuna nafasi ya kujiona upo juu sana. Hii inaweza ikakupunguzia kasi na kuona tayari umeshafika kileleni.

Kujilinganisha kunaweza kukukatisha tamaa. Unaweza ukaona wengine wapo juu sana ambako wewe hustahili kufikia. Hii inatokea pale inapoona kuwa ilibidi uwe na mafanikio ambayo mtu mwingine yamemfikia kumbe yako yalikuwa tofauti na hayo unayojaribu kujilinganisha nayo.

Kuna njia sahihi ya kulinganisha uwezo wako. Njia hii itakufanya uweze kujua uwezo wako halisi. Pia itakufanya kujua kiasi gani cha uwezo wako ambacho umekwisha kukitumia. Njia hii ni kulinganisha ulichokifanya na uwezo wako halisi. Ili kuwa sahihi katika hili huna budi kujua kusudi lako la kuwepo  hapa duniani. Unapofanikiwa kujua kusudi lako na kuanza kulitimiza, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuamsha uwezo wako na kufikia mafanikio makubwa.

Watu wengi wameshindwa kufikia mafanikio makubwa kwa sababu ya kutotambua kwa nini wapo hapa duniani na ambapo wanapojaribu kuiishi kwa nini hiyo ingewalazimisha kuamsha uwezo wao na kufanya zaidi ya sasa.

 Ni wakati wako sasa kutambua kusudi lako ili likusaidie kufanya makubwa hapa duniani. Kusudi lako limebebwa na kitu ambacho unakipenda kukifanya na unao uwezo wa kukifanya kwa viwango vya juu na urahisi ambao wengine hawawezi kuufikia. Hiki ni kitu ambacho upo tayari kukifanya hata kama hulipwi lakini kawa sababu utakuwa unatoa thamani kubwa kwa watu wengine, watakuwa tayari kukulipa. Kitu hicho ni nini?

Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI kimeelezea kiundani namna ya kutambua kusudi lako na kisha kuamsha uwezo wako na kufikia mafanikio makubwa. Pata nakala yako leo ili uanze kuishi kikamilifu leo na kufika mafanikio makubwa. Kitabu hiki kinauzwa sh. 10,000/. Kwa mawasiliano zaidi piga simu namba 0752206899 (Alfred Mwanyika).

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *