Usikubali Kwenda Na Mafuriko….
Mafuriko yakipita sehemu kuna uwezekano wa kuleta madhara. Madhara yatokanayo na mafuriko ni kama uharibifu wa miundombinu, vifo, upotevu wa mali nk. Matamanio ya watu wengi ni kuona mafuriko yanayopita hayaleti madhara yoyote kwenye maeneo yalikopita. Hii itakuwa salama kwenye maeneo yalikopita.
Mafuriko pia hutokea kwa watu, hizi ni changamoto ambazo mtu anazipata wakati akiendelea kuishi. Hizi ni changamoto ambazo mtu anazipata wakati anaendelea kutekeleza mipango yake ili kufikia maisha ya mafanikio. Changamoto nyingine huwa kubwa na chungu sana kiasi cha kumvuruga mtu kwenye kile alichokuwa anakifanya na baadaye kukata tamaa kabisa.
Kama ilivyo kwenye matamanio yako ya kutosombwa na mafuriko mvua ikinyesha, ndivyo inavyotakiwa kutamani na kufanya pale unapokumbwa na changamoto. Hakikisha husombwi na mafuriko ya changamoto. Maisha ya mafanikio makubwa yana changamoto kubwa na nyingi sana. Ili uweze kuyafikia mafanikio hayo, ni lazima uhakikishe unabaki salama na kuendelea na jitihada za kuyatengeneza mafanikio hayo mpaka uyapate.
Akili yako isiende na mafuriko. Chochote unachokifanya kinatokana na maamuzi unayoyafanya. Maamuzi sahihi hufanywa kwa kufikiri. Unapokutana na changamoto, hakikisha akili yako inabaki salama. Ukiruhusu akili yako ivurugike wakati wa kufanya maamuzi, utaishia kufanya maamuzi ya hovyo. Je hujawahi kuona mtu akiuza biashara yake kwa hasara baada ya kupata hasara? Je hujawahi kumuona mtu akichukua maamuzi ya kujiua baada ya kuwa na maisha magumu? Hakikisha akili yako haisombwi na mafuriko.
Misimamo yako isiende na mafuriko. Kuna viwango unavyovifuata kwenye kila eneo la maisha yako. Huu ni misimamo. Misimamo hiyo hupimwa kipindi cha dhoruba. Kila mtu anaweza kusema ana msimamo ambao ndiyo msingi wa maamuzi wako. Je huo msingi hauzolewi mafuriko ya changamoto yakikukuta? Hakikisha unaendelea kusimama imara pale unapokutana na changamoto. Msimamo ndiyo utakaokufikisha kwenye mafanikio makubwa.
Uvumilivu wako usiende na mafuriko. Changamoto za mafanikio huwa haziishi, usije ukaikabili moja ukajua umeshamaliza. Utayapata mafanikio yako kama utakuwa mvumilivu wa kuvuka vikwazo vyote mpaka pale utakapofanikiwa kupata unachokitaka. Ukipata hasara kwenye biashara mara ya kwanza kuna nafasi ya kupata hasara tena. Licha ya changamoto hizo, hakikisha unasonga mbele, ili inajitokeza tena isiwe na madhara kama ilivyokuwa mwanzo.
Biashara gani uliivunja baada ya kupata hasara au kuwa na mauzo kidogo? Mahusiano gani uliyavunja baada ya upendo wa mweza wako kuhisi umepungua? Kitu gani ulikiacha baada ya kuona huwezi kukifanya na hukutaka kujifunza? Kama hayo yalisimama katikati ya mafanikio basi hakikisha unarudi tena na kufufua vile vilivyokufa baada ya kupatwa na changamoto. Acha mafuriko yapite bali wewe endelea na safari yako ya kutengeneza maisha yako.
Changamoto zikikujia kwenye mbio za kutengeneza mafanikio; linda akili yako ifanye maamuzi sahihi, heshimu misimamo yako na vumilia ukijifunza na kuwa bora mpaka uyapate mafanikio yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz