Wewe Ni Samaki, Usimwigilizie Ndege Kuruka
Jambo moja ambalo lingemhakikishia samaki kushindwa maisha yake ni kutaka kuwa ndege. Kwa kutamani kuwa ndege, samaki angehangaika kutoka kwenye makazi yake ili aweze kuruka. Pia hata angefanikiwa kuruka, angefanikiwa kwa kiasi kidogo sana ukilinganisha na ndege. Kadhalika kitendo cha kuacha makazi yake, ingehatarisha maisha yake.
Ukisikia samaki ameacha kuogelea majini na badala yake anahangaika kujaribu kuruka utakuwa miongoni mwa watu wa watakaomshangaa na kumshauri samaki aachane na mambo hayo. Utajiuliza kwa ufundi wa kuogelea alionao samaki, kwa nini amefikiria kuanza kuruka na kuelea hewani?
Lakini kumbe kabla ya kumshangaa samaki inabidi ujishangae wewe kwanza, kwa sababu na wewe umeacha kufanya kile ulichoumbwa kukifanya na umetamani vya watu wengine.
Kama samaki alivyoumbwa kwa upekee wake wa kuishi majini na kuogelea na kupata mafanikio makubwa ndivyo ilivyo kwa binadamu. Kila binadamu ameumbwa kwa namna ya pekee sana inayomfanya binadamu mmoja kutofanana na binadamu mwingine yoyote.
Upekee huo unamfanya pia awe na uwezo wa kipekee ambao unamwezesha kufanya mambo makubwa na ya kushangaza. Ni mpaka pale atakapogundua upekee huo ndipo unapoweza kuishi maisha yake kwa kiwango anachostahili. Kupitia uwezo wa kipekee, dunia ilitarajiwa kuwa na watu wengi ambao wamefanya mambo makubwa ya kushangaza. Lakini hali imekuwa tofauti kwa sababu ni asilimia ndogo tu ya watu wamefanikiwa kuishi upekee huo na kutumia uwezo wao japo kwa 15%.
Sasa unaweza kujiuliza, licha ya binadamu kuwa na uwezo huo wa kipekee wa kufanya makubwa, kwa nini binadamu wengi bado wanaishi maisha ya kawaida? Sababu mojawapo ni watu kuacha kuishi maisha yao na badala yake kuishi maisha ya wengine. Huwezi kuishi maisha ya watu wengine halafu ukafanikiwa kuishi maisha yako halisi yaani yenye mafanikio makubwa. Watu kwa kujua au kutokujua wamekuwa wakiiga wengine wanavyoishi huku wakiamini binadamu wote ni sawa. Kwa kuamini hivyo imekuwa rahisi pia kuiga anachokifanya mtu mwingine akiamini atapata mafanikio makubwa.
Mtu unapoiga anachokifanya mtu mwingine, ni sawa na samaki anavyojaribu kuwa ndege. Unapoiga mtu mwingine unaishia kuwa mtu wa kawaida. Unaweza ukajitetea kuwa kuna mafanikio umeyapata, ni kweli lakini si kiwango ambacho ulistahili kukipata. Ukiona matokeo unayoyapata hayakushangazi wewe au dunia ujue ni ya kawaida tu.
Kuna mafanikio ambayo ungeweza kuyafikia kama ungefanikiwa kujua wewe ni nani na kuuishi upekee huo. Kuishi upekee wako ungeamsha uwezo wako wa kipekee ambao tayari upo ndani mwako tangu kuzaliwa. Uwezo wako wa kipekee umeambatana na vipaji vyako ambavyo vitakuwezesha kufanya mambo kwa viwango vya juu sana. Thamani kubwa na ya kipekee utakayokuwa unaipa dunia ndiyo itakayokurejeshea mafanikio makubwa maishani mwako.
Njia pekee ya kufikia mafanikio yako makubwa ni kurudi kwenye asili yako, yaani kuwa wewe. Kuwa wewe kunahusisha kufanya vitu vile ulivyoumbwa kuvifanya. Kama samaki anavyopata urahisi wa kuelea akiwa majini na sio hewani, ndivyo nawe unavyoweza kufanya mambo makubwa kwa urahisi ukiwa unaishi upekee wako.
Njia mojawapo ya kujua upekee wako ni kuusikiliza moyo wako. Moyo wako unakutambua vizuri sana, wewe ni nani? kwa nini upo hapa duniani? una nini cha pekee ndani mwako na nini unaweza kufanya kwa upekee mkubwa hapa duniani? Sauti ya moyo wako imefifishwa sana na sauti za dunia na ndiyo maana umekuwa unafanya unachoambiwa nje badala ya kile ambacho ungeweza kusikiliza ndani mwako.
Umesikiliza sauti za dunia kwa muda mrefu sasa, inatosha! Tenga muda na sikiliza moyo wako, utakutambulisha wewe na ulivyonavyo na kisha kukuongoza kuishi upekee wako ambao utakupa mafanikio makubwa unayostahili.
Kujua zaidi kuhusu upekee wako ambao ndiyo sababu ya wewe kuwepo hapa duniani, soma kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI. Kitabu hiki kimeelezea kiundani upekee wa mtu na jinsi ya kuuishi. Pata nakala yako sasa kwa kupiga simu namba 0752206899.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.
Mawasiliano:
Simu: 0752 206 899/0714 301 952
Email: alfred@amshauwezo.co.tz