Tone La Mvua Lisilokoma Hujaza Pipa


Categories :

Ni rahisi sana kulidharau tone la maji ya mvua kwa kuona si kitu. Kama kuna sehemu nyumba inavuja na tone moja linadondoka  kila wakati unaweza ukadharau ujazo huo na kuuamua kukinga kikombe tu. Lakini kama mvua itaendelea kunyesha bila kukoma, hata ukikinga pipa litajaa. Jambo kubwa litakaloamua pipa hilo kujaa, ni muda lakini pia kuhakikisha pipa linaendelea kuachwa kwenye uelekeo wa tone hilo.

Umekuwa ni utamaduni wa watu kudharau hatua ndogo na matokeo madogo wanayoyapata kila siku. Watu hufikiri ndoto na mipango mikubwa waliyonayo inaweza kutekelezwa mara moja tu. Wameendelea kuamini kuwa matokeo makubwa ya ndoto na malengo yao makubwa yatakuja mara moja

Dhana hii yakufikiri kuwa mafanikio makubwa yanakuja mara moja kama vile mvua kubwa inavyoshuka yamewafanya watu kudharau hatua na matokeo madogo. Ndiyo maana watu wamekuwa wakisikilizia sana bahati nasibu kwani michezo hiyo humpa mtu fedha nyingi mara moja. Japo pia hupotea mara moja. Pia imekuwa ni vigumu kwa mtu kuanzisha biashara ndogo na kuikuza kuwa kubwa kwa miaka mitano, kwani anaambiwa kuna biashara ambayo ukiifanya ndani ya miezi miwili tu unakuwa milionea.  Hii imekuwa ni sababu mojawapo ya watu kutapeliwa kirahisi.

Robert Collier anasema “Success is the sum of small efforts, repeated day in and day out” ikitafsiriwa kuwa mafanikio ni jumla ya jitihada ndogo ndogo zikirudiwa kila siku. Kama tulivyoona tone la mvua likiendelea kudondoka kwenye pipa bila kukata tamaa linavyoweza kujaza pipa hilo ndivyo ilivyo kwenye jitihada zako ndogo ukiendelea kuzifanya bila kukoma. Matokeo madogo unayoyapata kila siku yakitunzwa yatakusanyika na kutengeneza kitu kikubwa. Katika kuendelea kutekeleza mipango yako, matokeo yaliyokusanywa yataongeza nguvu kubwa katika kutekeleza mipango yako.

Kuna msemo  unasema safari ya maili elfu moja inaanza na hatua moja. Hata kama unatarajia mafanikio makubwa, yote yanabebwa na hatua unazochukua kila siku na matokeo  unayaoendelea kukusanya. Hivyo usizidharau hatua ambazo inabidi uzichukue kufikia mafanikio yako makubwa hata kama zitaonekana ni ndogo. Kwa kuwa hatua hizo ndogo zikirudiwa kila siku zitazalisha matokeo makubwa kadri muda unavyozidi kwenda.

Umeona jinsi hatu ndogo zinazochukuliwa kila siku zilivyo na machango kwenye kupata matokeo makubwa. Hivyo hata kama una lengo kubwa na la muda mrefu kwa mfano miaka mitano huna budi kuligawa katika vipande vidogo vidogo. Hakikisaha unapoligawa lengo hilo unakuwa na kitu cha kufanya kila siku kisha chukua hatua hizo bila kuacha. Katika maisha yako ya kutafuta mafanikio makubwa, ithamini siku kwani mipango yako yote uliyonayo itatekelezwa kwa mfulilizo wa siku kadhaa. Hivyo ili siku iwe na thamani kwako hakikisha unaipangilia vizuri ili kuweza kufanya yale uliyoyapanga siku hiyo kikamilifu.

Imekuwa rahisi kwa watu kupuuza matokeo madogo kwa mfano fedha ndogo. Kama mtu anafanya biashara na kupata faida ndogo, imekuwa rahisi kwake kutoithamini kwa kuona haiwezi kuwa msaada kwake. Ndugu! tumeona kuwa pipa litajazwa na tone moja la mvua linaloendelea kudondoka bila kukata tamaa. Hivyo fedha ndogo unayoendelea kuipata na kuikusanya ama kwa kuwekeza tena kwenye biashara au kuweka akiba itaongezeka na kuwa kubwa kadri muda unavyoenda. Kumbuka elfu kumi ambayo unaona ina thamani kubwa ni mkusanyika wa shilingi elfu moja unayoibeza kwa siku kumi tu. Kadhalika milioni moja unayoithamini sana ni mkusanyika wa shilingi elfu kumi unayoidharau kwa siku mia moja tu.

Mafanikio makubwa unayoyasubiria kwa hamu yatapatikana kwa jitihada ndogo na matokeo madogo ya kila siku. Kila siku jiulize ni hatua gani unaenda kuzichukua siku hiyo kwa ajili ya malengo yako makubwa? Pia tambua matokaeo ambayo utaenda kuyapata siku hiyo. Ukishajua hatua za kuchukua na matokeo unayoenda kupata, kuwa mwaminifu kwa kuchukua hatua hizo kikamilifu na pia kutunza matokeo hayo. Hivyo ndivyo utakavyoweza kufikia mafanikio yako makubwa.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *