Pandisha Viwango Kufikia Utajiri.
Hatua ya mafanikio ya maisha uliyofikia ni kwa sababu ya viwango ulivyojiwekea maishani mwako. Viwango hivyo ndiyo ndivyo vinavyoamua ufanikiwe kiasi gani kwenye kila nyanja ya maisha yako. Viwango hivyo ndivyo vinavyoweka ukomo kwenye mafanikio unayoyapata, hii ndiyo sababu ya kwa nini muda umezidi kwenda lakini bado upo pale pale.
Viwango hivyo ulivyojiwekea vimeanzia kwenye akili yako. Kile ambacho unakiamini kuwa unastahili na unaweza kukipata ndicho unachokipata maishani. Kama akili yako inaamini wewe ni viwango vya laki, inakuwa ngumu sana kupata milioni. Hata ikatokea kwa bahati mbaya ukapata milioni, suala la muda, utarudi tena kwenye kiwango cha laki. Kama akili yako haiamini kuwa unaweza kuwa bilionea, basi jitihada zote zitakuwa zinaishia kwenye milioni.
Ndiyo maana kuna watu wamewahi kupata fedha nyingi kwa mkupuo ambazo zilikuwa juu ya viwango vyao na baada ya muda mfupi wakapoteza zote. Kuna watu wameshawahi kushinda bahati nasibu na kupata fedha, watu wakaamini kuwa wameshashinda maisha, lakini baada ya muda mfupi fedha zote zikaisha na wakarudia maisha yao ya kawaida.
Ndugu uwezo wako haujaishia hapo, unayapata matokeo hayo kwa sababu ya viwango ulivyojiwekea. Huwezi ukaenda mbali ya hapo mpaka utakapoiruhusu akili yako kuamini viwango vya juu zaidi. Ni sawa na mbuzi aliyefungwa kamba kwa ajili ya malisho, hawezi kwenda kula mbali zaidi ya urefu wa kamba yake. Ili aweze kwenda mbali zaidi, inabidi aongezewe urefu wa kamba yake au afunguliwe na kuachiwa huru.
Kupandisha viwango ni kukubali kuishi maisha ya aina nyingine. Haya ni maisha ambayo hayafanani na maisha ambayo umezoea kuishi na kupata matokeo ulidumu kwa muda mrefu. Kupandisha viwango ni hatua za kutumia uwezo wako kwa kufanya vitu vigeni au vilevile kwa viwango vya juu zaidi. Zifuatazo ni hatua za kuchukua ili kuweza kupandisha viwango vya mafanikio yako:
Amini kuwa unaweza kupata matokeo zaidi ya hayo: Inafahamika kuwa hata watu ambao tunaona wamepata matokeo makubwa wametumia sia zaidi ya 15% ya uwezo wao. Jiulize wewe ndugu yangu umetumia kiasi gani kwa matokeo uliyoyapata. Kumbe kuna nafasi ya kupanda juu zaidi ya hapo ulipofika. Hivyo hatua ya kwanza ili uweze kuongeza viwango vyako ni kuvunja imani uliyokuwa nayo kuwa umeshafika mwisho. Bado kuna nafasi ya kufanya zaidi ya hapo. Akili na moyo wako viamini hivyo. Mwimbaji na mwanamitindo Mrilyn Munroe alisema ‘’The sky is not the limit. But your mind’’ akimaanisha kuwa anga haliwezi kuwa kikwazo bali akili yako.
Tathimini ulipo sasa: Baada ya kuamini kuwa una nafasi ya kwenda mbali zaidi huna budi kufanya tathimini kujua ulipo sasa. Kama ni kiuchumi je wewe ni wa elfu, au laki, au milioni au bilioni au trilioni. Kama kwenye kazi, je kiwango ulichofikia umeridhika nacho, je hatua uliyofikia ni maboresho ya mwisho? Je upo kwenye hatua gani kimahusiano? Unashirikiana vipi na watu wanaokuzunguka? Vipi kuhusu maendeleo yako binafsi, ufahamu wa vitu ukoje?Kuna maeneo kadhaa ya kujifanyia tathmini na kujua mahali ulipo ili kujua wapi unaweza kuelekea pia
Weka viwango vya juu zaidi: Baada ya kufanya tathimini, hatua inayofuata ni kuweka viwango vya juu kuliko ulipo sasa. Kama tulivyoona hapo juu kuwa hakuna kitu kinacho kuzuia kupata chochote isipokuwa kiasi utakachopimiwa na akili yako. Huu utakuwa muda wa kujipimia kiasi kukubwa kuliko ulicho nacho sasa. Mwandishi Napoleon Hill aliandika kuwa “Whatever Your Mind Can Conceive and Believe, It Can Achieve.” Akimaanisha kuwa chochote ambacho akili yako inakiridhia kitafikiiwa. Akili ni yako, na kazi ambayo itapanga itafanikiwa kwa sababu tayari uwezo huo upo ndani yake. Usiogope kuweka viwango vikubwa, uwezo wa kuvifikia viwango hivyo upo, wewe iruhusu akili yako iamini.
Weka mikakati ya kufikia viwango utajiri wako;
Viwango ulivyoweka ni malengo ambayo yanahitaji mikakati ili kuyafikia. Kwa sababu viwango vya sasa ni vikubwa kuliko ulivyozoea, unahitaji kuweka nguvu zaidi na kufanya tofauti na mazoea. Ili mkakati huo uweze kutimia huna budi kufahamu kilicho sahihi kufanya ili uweze kufika viwango vya juu kisha kuweka nidhamu ya hali ya juu ya kazi.
Vile ulivyozoea kufanya ndiyo kumekufikisha hapo ulipo, ili uweze kupata matokeo ya utofauti huna budi kufanya tofauti na mazoea. Ndiyo maana mwanasayansi nguli Albert Einstein anasema “Insanity is doing the same thing over and over and expecting different results.” Akimaanisha kuwa wazimu ni kufanya jambo kitu hicho hicho kila wakati na ukitarajia kupata matokeo tofauti. Hii ni kauli ambayo inakukumbusha kuwa itakulazimu kubadilika ili uweze kupata matokeo baadaye kuweka viwango vya juu. Kiwango gani kikubwa unakiweka leo?
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz