Kwa Nini Unajifungia Mwenyewe?


Categories :

Binadamu ameshindwa kutumia hazina kubwa ya uwezo ndani yake kwa sababu ya ukomo anaojiwekea. Wapo watu wanaoendelea kuendesha magari ambayo wao wanatafsiri ni ya kawaida huku wakiishia kutamani magari mazuri. Ukimwuliza kwa nini hamiliki gari hilo anasema yeye hufanana na gari hilo. Gari hilo zuri ni watu wa daraja fulani ambalo yeye hayumo?

Wewe wa daraja gani?

Tungeweza kuangalia mifano mingi sana ambayo inaonyesha ni kwa kiasi gani watu wanajiwekea ukomo. Kitu ambacho unaweza kukifanya ni kile ambacho akili yako inaweza kukikumbatia. Kumbe matokeo unayoyapata unastahili kabisa kwa sababu ndiyo kiwango ambacho umekipangia akili yako na akili yako ikakikumbatia.

Daraja ulilopo linaweza kuwa siyo unastahili lakini umejistahilisha. Huwezi kutoka kwenye daraja hilo mpaka pale utakapotoa ukomo huo uliojiwekea. Usitarajie kupata makubwa au kutenda miujiza kama akili yako haioni miujiza mbele yako. Matshona Dhliwayo anasema ‘’Maisha hayajakuweka ukomo kwenye yale unayoyapata tofauti na ukomo uliojiwekea mwenyewe’’ Kwa hiyo kama kuna mtu wa kumulaumu kwa yale unayopata basi wa kwanza ni wewe mwenyewe.  Maana ndiye uliyeweka mipaka hiyo.

Nani amekuweka kwenye daraja hilo?

Tumeona kuwa mtu wa kulaumiwa kwa matokeo unayoyapata ni wewe mwenyewe. Kutokana na uliyoambiwa, ona na kufundishwa ukapata taswira wapi inabidi uwe. Changamoto hii unaanza pale unapoanza kutafakari na kuelewa unachoona, ambiwa na kufanya.  Ulipokuwa mtoto uliamini kila kitu kinawezekana.  Ndiyo maana uliamini chochote utakachomuomba mzazi atakupa. Na dhana hii ilikusaidia kwani kuna muda mazazi alilazimika kukopa hata fedha ili akununulie kile ulichomlilia kwa imani kwamba mazazi anaweza kukununulia.

Shida ilianzia pale ulipoambiwa wewe huna akili,  na ukaamini. Hivyo umekuwa ukijiepusha sana na vitu ambavyo wanasema ili uweze kufanikiwa inahitaji akili kubwa. Shida iliendelea pale ulipoambiwa mambo makubwa yanafanywa na watu wa kabila au rangi ya ngozi fulani na wewe ukaamini. Ndiyo maana mpaka leo unaishia kwenye utajiri wa kawaida na maisha ya kawaida.

Mtu sahihi wa kukusaidia  kujinasua na  mtego huu wa ukomo ni wewe mwenyewe. Uwezo ulionao ndani yako ni maradufu ya kiwango ulichojiwekea. Uwezo wako wa ndani hauna mipaka. Unaweza ukafanya na kupata matokeo kwa kiwango kile unachokifikiria na kukiamini. Mtu wa laki huwezi ikawa milionea kama hutatoa ukomo wa laki. Kadhalika mtu wa milioni huwezi ikawa niliongea kama hutavuka kwenye ukomo wa milionea.

Hata kama utavuka ukomo huo kwa bahati mbaya, ni jambo la muda tu, utarudi kule ulikostahilisha.

Hata kama kwa bahati mbaya, bilionea ataporomoka akawa mtu wa laki,  ni jambo la muda ataurudia ubilionea wake.

Jim Kwik kwenye kitabu chake cha limitless anasema “Usiminye ndoto zako zifanane na uhalisia wa sasa” Naamini maishani mwako umekuwa na ndoto kubwa ya kufikia mafanikio makubwa. Lakini ndoto hizo zimekuwa zikiyeyuka baada ya kuangalia uhalisia. Umekuwa ukiangalia kilichopo kwenye jamii, watu wanafanya nini na wanataka nini.

Kulingana na changamoto zilizopo kwenye jamii imekuwa ukilazimisha na kujiaminisha kuwa unayoyafikiri huwezi kuyakamilisha.

Hali ya sasa sio daraja lako, daraja lako ni la juu sana. Jukumu la kwanza ni wewe kutoa ukomo wa mafanikio uliojiwekea kwenye kila eneo la maisha yako. Anza kuona makuu na miujiza kwenye ndoto zako. Kwa kufanya hivyo utaamusha uwezo wako halisi ulio ndani yako.

Tafakari kwa kina kama kungekuwa hakuna kikwazo chochote, ni mtu wa namna gani ulitamani uwe? Kiasi gani cha fedha ungeridhika kuwa nacho? Wapi ungetamani ufike kabla hujaaga dunia? Haya yote unaweza kuyapata kama utatoa ukinzani na mipaka uliyojiwekea akilini mwako. Unaweza kuwa mtu yoyote unayetaka; acha kujifungia kuwa unayetaka.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *