Mruhusu Huyu Aishi Maisha Yako.


Categories :


“Hata kama mtasimama watu wengi, bado kila mtu atatengeneza kivuli chake”

Ukisimama sehemu yenye mwanga upande mmoja nyakati za usiku kivuli kitatokea. Mtu mwingine akisogea mahali hapo, kivuli kingine kitajitokeza. Hata pale watu kumi watakaposogea bado kila mtu atatengeneza kivuli chake. Hii inamaanisha kuwa hakuna namna yoyote mtu anaweza kuzalisha kivuli kwa niaba ya mwingine.

Hii ni ishara kuwa kila binadamu ana kitu cha pekee ndani yake ambacho hakiwezi kwenda kwa mtu mwingine . Kama ambavyo una uwezo wa kuzalisha kivuli chako mwenyewe ndivyo unavyoweza kusimama peke yako hapa duniani kutengeneza maisha yako ya mafanikio makubwa mno.

Ndani yako una uwezo wa kipekee wa kufanya chochote bila ya kuazima kwa mtu mwingine . Kila mtu ana uwezo huo kama ambavyo kila mtu alivyozalisha kivuli chake mwenyewe . Usione kama watu fulani wamependelewa uwezo na kustahili kufanikiwa, la hasha bali kila mtu , ukiwemo wewe unaweza kufanikiwa.

Uliumbwa ukiwa umekamilika kwa kila kitu, huhitaji kukopa uwezo kwa mtu mwingine ili uweze kuishi kwa mafanikio makubwa, bali ni kuamsha kile kichopo ndani yako na kutumia kupata mafanikio makubwa.

Kama kila mtu anavyoweza kuzalisha kivuli chake, ndivyo ilivyo kwenye ndoto za wanadamu. Kila mtu anaweza kutengeneza ndoto yake na kukiishi kikamilifu. Kama sasa huishi ndoto yako bado tambua unasaidia kukamilisha ndoto ya mtu mwingine. Mtu sahihi wa kuishi maisha yako kikamilifu ni WEWE MWENYEWE. Ndoto yako utaanza kuiishi lini?


Hakuna mtu mwingine anayeweza kuishi ndoto yako kwa niaba yako. Hakuna mtu anayeweza kutumia uwezo wako mkubwa uliolala ndani yako kwa siku nyingi bila kuuamsha. Hii imekuwa sababu ya watu wengi kufa na hazina zao angali bado hawajazitumia. Ndiyo maana wanasema kuna utajiri mkubwa sana umelala makaburini

Kuna watu wamekufa na kuzikwa bila kuandika kitabu ambacho labda kingekuwa mwongozo mzuri wa kuishi maisha yao kikamilifu. Kuna watu wamekufa na mawazo mazuri ya biashara ambazo zingeacha utajiri mkubwa kwa watu wengine. Wapo waliokufa na nyimbo nzuri bila kuombwa wao kurekodiwa ambazo wangeziimba zingekuwa viburudisho kwa watu.

Ndugu! Una kitu kikubwa ndani yako na cha kipekee. Kitu hicho ni uwezo wako kipekee. Bahati nzuri bado upo hai, hii ni fursa ya kufanya vingi vilivyoshindikana kwa muda mrefu. Una fursa sasa ya kuanzisha mipango ya kupata kile unachotamani kukipata siku nyingi. Uwezo huo upo ndani yako, unasubiri nini kuanza kuutumia?

Kaa chini na tafakari picha kubwa ya maisha yako unayotaka itimie, weka mipango na anza kuitekeleza mara moja. Je ni biashara gani hiyo? Je ni mahusiano gani hayo? Je ni utajiri kiasi gani huo? Vyote vipo ndani yako, vipakue!


Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *