Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Kesho Yako Leo.


Categories :

“Msitu wa miti unaouona leo ni matokeo ya miche iliyopandwa na kulindwa kwa miaka mingi hapo nyuma”

Maisha yako ya leo sio ya leo bali ya miaka mingi ya nyuma. Kile ulichokuwa unakifanya miaka kadhaa iliyopita ndicho kilichokupa maisha yako ya leo. Kama unafurahia maisha yako leo ujue kwa asilimia kubwa sio kwa sababu unayoyatenda sasa bali yale uliyokuwa unafanya muda uliopita. Kadhalika kama unajutia maisha haya unayoyaishi sasa, tambua ni kwa sababu ya yale uliyoyatenda muda uliopita.

Kanuni ya kisababishi na matokeo inasema kwenye kila matokeo unayoyapata kuna kisababishi kinacholeta matokeo hayo. Hivyo hakuna kitu kinachotokea chenyewe tu bali kwa kusababishwa. Matokeo ya maisha ya jumla huchukua muda mrefu, hivyo haya ya sasa ni matokeo ya yale uliyoyatenda siku nyingi zilizopita.

Kama bado upo hai, una maisha mengine yajayo. Una nafasi ya kuyatengeneza maisha yajayo unayoyataka. Nafasi hiyo ya kuyatengeneza maisha hayo unayo sasa na si muda huo ukifika. Maisha yako ya kesho yanajengwa leo na siyo kesho hiyo hiyo. Kumbe unaweza kutabiri maisha ya mtu yatakavyokuwa kwa kuangalia anachokifanya leo.

Ndugu! Usiendelee kulia kwa maisha magumu uliyonayo sasa, bali ni muda sasa wa kujenga maisha yako ya kesho. Mchora ramani ya nyumba huwa na picha kamili ya nyumba itakayojengwa hata kabla ya kuonekana kwenye karatasi. Hivyo hutangulia kuiona nyumba hata kabla haijajengwa. Ndivyo ilivyo kwenye ujenzi wa maisha yako, huna budi kuyaona maisha yako ya mbele hata kabla hujayafikia. Maisha ya kesho yanaonwa leo. Hivi ndivyo unavyoweza kujenga maisha yako ya kesho kwa mafanikio makubwa;

Yaone maisha yako ya kesho leo. Kama mchoraji anavyoiona nyumba hata kabla hajaichora kwenye karatasi, ndivyo na wewe unavyotakiwa kuyaona maisha yako ya baadaye leo. Unataka uwe na nini hapo baadaye? Unataka kuwa nani hapo baadaye? Unaona ukiwa umepiga hatua gani baada ya miaka mitano ijayo? Ona picha kamili ya maisha hayo. Huwezi kujenga kitu ambacho hukioni kwenye fikra.

Yaweke malengo maisha hayo. Baada ya kuwa na picha kamili ya maisha unayotaka, sasa unakuwa wakati wa kuwekea mikakati ya kuileta picha hiyo kwenye uhalisia. Weka malengo ya namna ya kuyatengeneza maisha hayo. Malengo yako yatakuwa ya muda mrefu, wa kati na mfupi. Kwenye kila lengo kutakuwa na hatua za kuchukua na muda unaotarajia matokeo.

Weka kazi leo juu maisha yako ya kesho. Kama ilivyo kwenye sheria ya kisababishi na matokeo, hakuna picha yoyote itakayotokea kwenye uhalisia bila kuweka kazi. Hata kama utaweka  mipango mizuri kiasi gani, bila kazi hakuna kinachoweza kutokea. Hakikisha kila siku kuna kitu unakifanya kwa ajili ya kesho yako.

Tathmini mwelekeo wa kesho yako. Kujua kama  mipango yako itakupa matokeo unayotaka huna budi kuhakikisha unafanya tathmini mara kwa mara. Hii itakusaidia kujua kama unakua au unakufa. Pia itakuonyesha maeneo unayokwama na kisha kufanya marekebisho na kufanya vizuri zaidi.

Kesho yako ipo mikononi mwako sasa. Miaka ijayo utakuwa unafurahia au kujua yale unayoamua na kufanya au kutokufanya leo. Hakuna kitakachotokea bila kukifikiria na kukiamini. Weka mipango kwenye picha unayoiona ya maisha ya kesho na hakika kesho yako itakuwa bora kuliko leo.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *