Tambua Iliko Thamani Yako Kubwa Isiyoonekana.


Categories :



Vitu vikubwa na vyenye nguvu kubwa huwa havionekani kirahisi kwa macho. Ni mpaka matokeo yake ndipo unajua kuwa kulikuwa kuna nguvu kubwa.

Angalia umeme, huwezi kuuona kwa macho kirahisi lakini matokeo ya umeme kila mtu anayaona. Umeme unawasha taa usiku na kutupa mwanga. Umeme unaendesha mitambo mikubwa kama mashine za kunyanyua mizigo mikubwa.

Nguvu ya mawimbi. Mawimbi hatuyaoni kwa macho lakini yamekuwa yakileta matokeo makubwa ambayo macho yetu yanaweza kuona. Nguvu hii imeleta matokeo makubwa sana katika mawasiliano. Sasa una uwezo wa kuwasiliana na mtu mwingine popote duniani.

Ndivyo ilivyo kwenye uwezo wa mtu. Thamani kubwa ya uwezo wa mtu haipo kwenye mambo ya kawaida ambayo mtu anafanya kwa akili ya kawaida. Uwezo huo haupo kwenye mambo ambayo yanonekana na macho ya kila mtu. Uwezo huo upo kwanza ndani ya mtu, na mwanzoni hauonekani kwa kila mtu mpaka anapoanza kuzalisha matokeo.

Unaweza ukajiuliza kwa nini watu wengi wamekuwa wa kawaida wakifanya vitu vya kawaida? Naita vya kawaida kwa sababu hakuna upekee, yaani ni mambo mtu mwingine anaweza akafanya na akapata matokeo kama yako. Sababu kubwa ni kuwa watu wamefanya mambo mengi kwa kawaida yaani kwa namna ya nje nje. Namna hii sio ile ya nguvu iliyojificha ndani yao. Una nguvu nyingine iliyojificha ndani yako ambayo haionekani na ndiyo inayoweza kuleta matokeo makubwa katika maisha yako.


Nguvu hiyo imejificha wapi?

Kuna viungo vingi sana mwilini mwa binadamu. Japo vyote ni muhimu kuwepo mwilini, umuhimu huo umetofautiana. Unaweza ukaishi na jicho moja au bila macho. Unaweza kuishi bila mikono au miguu. Lakini huwezi kuishi bila moyo, ubongo, mapafu au figo.

Tafakari….. vitu unavyoweza kuishi bila kuwa navyo ni rahisi kuviona na kuvitukuza sana. Kila mtu anaweza akaona macho yako, mi mikono na miguu yako. Lakini vitu vile ambavyo huwezi kuishi bila hivyo vimefichwa ndani sana, havionekani kirahisi kwa macho. Angalia ubongo ulivyofichwa na fuvu kichwani, moyo/mapafu na mbavu.



Thamani kuu anayoweza kuitoa mwanadamu ipo moyoni mwako. Moyo ulijificha na kutoonekana kirahisi ndiko thamani ya mtu iliko.
Ukizama huko na kujua hasa kilichopo ndani yako, ndipo unapoweza kutumia uwezo zaidi ya kawaida. Ukifanikiwa kutumia uwezo huo wa kipekee ambao moyo wako utakunong’oneza utapata matokeo makubwa unayostahili.

Kuishi maisha ya kutoka moyoni ni kukubali au kuchagua kuishi kusudi. Huwezi ukaishi kusudi halafu ukapata matokeo ya kawaida.
Wale unaowaona wamefanikiwa kwa kufanya mambo makubwa hapa duniani wamekubali kuishi kusudi kikamilifu. Hawa wamekubali kusikiliza mioyo yao kuwa nini inayo na kujitoa kuishi kusudi hilo

Unausikiliza moyo wako?

Kama ulivyoona thamani kubwa ya maisha yako imejificha ndani yako. Ipo ndani ya moyo wako. Ni watu wachache sana wanapata nafasi kujua thamani hiyo iliyo ndani yao.
Hawa ni watu ambao wana utulivu wa kusikia kutoka mioyoni mwao.

Huwezi ukausikia moyo kwenye kelele.

Tunaishi kwenye dunia yenye kelele nyingi sana. Tangu unaamka mpaka unaenda kulala unapigiwa kelele. Umewaachia watu wakuambie wewe ni nani badala ya moyo wako kukuambia ukweli wewe ni nani. Maoni ya wengi juu yako ni kuwa wewe ni wa kawaida . Huna tofauti na wengine.

Hivyo ili ujue wewe ni nani unahitaji utulivu . Tenga muda wa kuwa peke yako , sikiliza kwa ukaribu moyo wako, una ujumbe wa wewe ni nani na utajiri ulio nao ndani yako.

Usiendelee kufanya chochote unachokiona na kinachoonwa na kufanywa na mtu yoyote. Ukuu wako upo kwenye kile kisichoonekana kirahisi na kila mtu yaani moyoni mwako. Usikilize moyo wako, utii na utafanya mambo makubwa ambayo yataishangaza dunia.

Tenga muda leo kwa kukaa sehemu yenye utulivu, sikiliza moyo wako ukikuambia wewe ni nani? Una upekee gani ndani yako? Kitu gani unaweza kukifanya kwa upekee? Kisha anza kukifanya hata kwa hatua ndogo.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *