Mafanikio Yako Yanaanza Leo.


Categories :



“Safari yako ya miaka mia moja inaanza na leo”


Una ndoto kubwa ambazo unatamani uzifikie kwenye maisha yako. Yamakini ili kutimiza hizo ndoto hizo tayari umeshaweka malengo ya kuyatimiza kwa kipindi fulani. Watu wengi pia wamekuwa wakiweka malengo kama wewe, lakini ni asilimia ndogo sana ya watu waliofanikiwa kuzifikia ndoto zao kupitia malengo wanayoweka.

Kuna siri moja ambayo watu wengi wamekuwa hawaifahamu ambayo imesababisha kutokufikia ndoto zao. Kama na wewe umekuwa miongoni mwa watu hao basi baada ya kusoma hapa utajua siri hiyo na kutoka hapo ulipokwama.
 

Siri hiyo ambayo imewasaidia wengi inaweza kukusaidia na wewe. Siri hiyo ni mafanikio ya siku, ndiyo mafanikio ya siku. Unapokuwa na ndoto za kuzitimiza maishani mwako, unakuwa na picha ya jinsi matokeo yatakavyokuwa na pia hatua utakazokuwa unachukua. Katika picha hiyo ni rahisi kuona matokeo ya ndoto zako yapo mbali . Pia unaweza ukaona kuwa hatua za kuchukua ili kuweza kufikia malengo hayo zipo mbali sana. Lakini matokeo makubwa yoyote unayoyaona yametokana na jinsi watu walivyofanikiwa kuiishi siku kwa mafanikio.


Miaka inaundwa na miezi, miezi inaundwa na majuma na majuma yanaundwa na siku. Kufanikiwa au kushindwa kunategemea namna unavyoiishi siku, kumbuka ni siku ya leo ndiyo una uhakika nayo. Yale unayofanya leo ndiyo yatakayoamua hatima ya maisha yako yajayo. Hata kama ndoto zako ni kubwa kiasi gani na kuwa zitachukua miaka mingi, lakini siri kubwa ya mafanikio ya miaka hiyo mingi ni ipo kwenye namna unavyoiishi leo.

 

Ili mipango mkubwa uliyo nayo iweze kutekelezwa ni lazima igawanywe na kueleweka ni kitu gani kinachoenda ndani ya siku. Baada ya leo kukamilika itakuja leo mpya ambayo ni kesho kukupa nafasi ya kurudia kufanya uliyokwisha kufanya na kwa kiwango cha juu zaidi. Kadri leo zinavyojirudia na kufanikiwa kuziishi kwa mafanikio ndivyo unavyotengeneza mafanikio yako makubwa. Unavyoamua kuiishi leo ndiyo kioo cha mafanikio yako ya miaka kumi ijayo.

 

Lengo kubwa ulilonalo huna budi kuligawa kwenye vipande. Gawa lengo lako la miaka kumi kwenye miaka mitano , halafu mwaka , miezi, juma na baadaye siku. Kwenye ndoto unazofanyia kazi ni lazima uhakikishe unajua ni kitu gani unaenda kufanyia kazi kwa siku ya leo. Hivyo kila unapoamka asubuhi hakikisha umejua ni kitu gani unaenda kukifanya siku ya leo.

Rober Collier alisema“Success is the sum of small efforts, repeated day in and day out” akimaanisha kuwa mafanikio ni jumla ya nguvu ndogondogo zinazorudiwa kila siku. Kumbe mafanikio makubwa unayoyatamani hayajengwi kwa mara moja bali kwa kuweka nguvu na kupiga hatua kila siku.

Baada ya kujua siri hii kubwa ya maisha ya mafanikio makubwa ya kuiishi leo kikamilifu hatua inayofuata ni kujipanga na kuona ni kwa namna gani unaiishi leo kikamilifu. Zifuatazo ni njia za kuiishi leo kikamilifu;

Chagua kitu kimoja cha kufanya kila siku.

Kama tulivyoona kuwa mafanikio makubwa maishani mwako hujengwa na mafanikio yako ya siku, huna budi kutafuta kitu ambacho utakifanya kila siku kwa uaminifu mkubwa. Je ni biashara ambayo itakupa faida kila siku hata kama mwanzoni itakuwa ndogo. Je ni kuweka akiba kila siku kwenye kipato unachokipata? Je ni kujifunza jambo jipya kila siku?

Amka mapema

Siku ya leo ambayo umeipata ni muda maalumu kwako ambao umeupata. Leo ni siku ambayo una uhakika nayo. Jana imeshapita na haiwezi kurudi tena, hata kesho huna uhakika nayo. Njia moja wapo ambayo unaweza kuitumia kuiishi leo vizuri ni kuwahi kuamka. Faida mojawapo ya kuwahi kuamka ni kupata utulivu. Moja ya kitu adimu katika nyakati hizi ni utulivu. Hii imesababishwa na kuwa na vyanzo vingi vya kelele kama vile mitandao ya kijamii, vijiwe, jamii nk.

Ili upate muda mzuri wa utulivu huna budi kuwahi kuamka. Ukifanikiwa kuamka saa moja au masaa mawili kabla ya watu wengine kuamka utaweza kupata muda wa utulivu wa kutafakari kuhusu uwepo wako hapa duniani na pia kuipangilia vizuri siku yako. Ukiwahi kuamka asubuhi unaweza unapata muda tahajudi/sala ambayo ni muhimu sana katika kuleta utulivu wa akili na roho. Pia unaweza kutumia muda huo kufanya mazoezi na kuimarisha afya. Unaweza kutumia muda wa asubuhi kusoma mambo muhimu kuhusu taaluma na kazi yako.

Kutoahirisha.

Moja ya sumu kubwa ya watu kutofikia mafanikio makubwa wanayoyataka ni kuahirisha mambo. Watu wengi ni wazuri sana wa kupanga mipango tena ile mizuri. Lakini utekelezaji unapofika wengi wamekuwa na sababu nyingi. Na ili kujifariji, wamekuwa wakisema watafanya kesho. Ili siku yako iwe ya mafanikio makubwa hakikisha unajenga nidhamu kubwa ya kufanya kile ulichokipanga kukifanya siku hiyo bila kuahirisha.

Ndugu mafanikio yako yamebebwa na hatua unazozichukua kila siku. Licha ya matokeo madogo unayoweza kuyapata, kadri unavyoendelea kukusanyika ndivyo unavyokuwa kwenye nafasi nzuri ya kufikia mafanikio makubwa. Changua jambo moja la kuanza nalo na lifanye kila siku kwa uaminifu.


Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *