Kwa Nini Umechoka Ungali Huna Matokeo?


Categories :

Mtoto mdogo huamka asubuhi akiwa hajui siku hiyo atafanya nini. Hivyo akiachiwa ataanza kugusa na kufanya chochote kitakachokuja mbele yake. Mpaka jioni inafika, mlezi akiulizwa mtoto amefanya nini leo, ni vigumu kueleza ni kitu gani hasa mtoto amefanya. Hii ni kwa sababu ya uwingi wa vitu ambavyo mtoto anavifanya tangu anaamka mpaka anaenda kulala. Licha ya kutokujua kwa dhati ni kitu gani mtoto amefanya siku hiyo, huonekana akiwa amechoka sana.

Mambo haya unajua yanafanywa na watoto tu ukiamini ndiyo kazi yao katika umri huo. Lakini na watu wazima wamekuwa wakifanya haya yanayofanywa na watoto. Unaweza ukajiuliza ni kwa namna gani mtu mzima atumiae muda wake tangu asubuhi mpaka jioni au wiki moja mpaka nyingine au mwaka mmoja mpaka mwingine kama mtoto mdogo? Lakini umekuwa ukifanya hayo kwa namna unavyoyaendesha maisha yako.

Umeyafanya hayo kwa kukosa kitu kimoja au vichache vya kujikita na kuvifanya hivyo mpaka vikupe majibu. Kwa kukosa kitu cha kubobea, umekuwa ukifanya chochote kinachokuja mbele yako. Kila fursa uliyoiona na kuisikia umeiona ni ya kwako na hukutaka kupitwa nayo.

Umekuwa ukianzisha jambo na kuweka nguvu, muda na umakini wako, lakini kabla hujafika mbali umesikia kuna kitu kingine ambacho kinalipa sana, ukaona kisikupite ukaanza kukifanya na hicho. Jambo hilo la pili umeanza kulifanyia kazi hata kabla ya la kwanza halijafika mbali. Kila siku fursa zimekuja mbele yako, na kuona unaweza kufanya vyote, na kwa sababu ya kuzidiwa, umekuwa mtu wa kugusa mambo na mara nyingine kuyaachia njiani. Hii ndiyo sababu ya wewe kutokuwa na matokeo makubwa ya kujivunia licha ya kufanya kazi muda mwingi.

Kutaka kuwa kwenye kila fursa ndiko kulikokuchosha. Unaona umekuwa ‘bize’ kwa muda mrefu sana, lakini hukioni cha maana ulichokifanya. Siku yako imekuwa bize sana, unaondoka asubuhi na kurudi usiku ukiwa umechoka, ukijiuliza umefanya nini siku hiyo, unakosa majibu ya moja kwa moja. Miaka mingi imepita tangu ulisema unaanza kusaka mafanikio, lakini ukipiga hesabu umepata au unatarajia nini, huna jibu. Ndugu, hapa umefanana na mtoto ambaye toka asubuhi mpaka jioni yupo bize, lakini ni vigumu kumuelezea ni kitu gani hasa amefanya.

Wakati umefika sasa wa kuchoshwa na jambo moja na si kila jambo. Chagua kitu kimoja ambacho utaelekeza nguvu, muda na umakini wako wote na kubaki huko mpaka upate matokeo unayotarajia. Kutawanya nguvu kwa kutaka kufanya kila kitu ndiyo kunakokuchosha licha kupata matokeo kidogo na kuishia kuwa wa kawaida. Kitu gani unakipenda kukifanya kwa moyo wako wote? Tengeneza ndoto yako kubwa kwenye kitu hicho kisha bobea kwenye jambo hilo mpaka likufikishe kwenye mafanikio makubwa.

Angalizo! Utakapoamua kuchagua jambo moja la kufanya, njiani utakutana na fursa nyingine nyingi ambazo zitakutamanisha na kuona hizo zinalipa zaidi ya kile unachokifanya, usihangaike nazo kwani zitapunguza umakini kwenye eneo unalotaka kubobea. Kadri unavyoendelea kung’ang’ana na jambo moja ndipo unapozidi kubobea kwenye jambo hilo. Unapobobea kwenye jambo, unakuwa kwenye nafasi kubwa ya kutoa thamani kubwa kwa watu wengine na wao kukupa chochote unachotaka.

Je unachagua kubobea kwenye biashara gani? Je unachagua kubobea kwenye fani gani? Je unachagua kubobea kwenye huduma gani? Je dunia ikutambue kwa jambo gani? Chagua eneo moja na hakikisha unazama huko na kutoa thamani kubwa ili hata kama utachoka utajua na kuridhika na kile kinachokuchosha.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *